Na. Edward Kondela
Wafugaji katika Kijiji cha Matanzi kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, wametakiwa kutunza mradi mkubwa wa maji uliojengwa na serikali ikiwa ni moja ya njia ya kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa ajili ya mifugo yao.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura, amesema hayo (08.09.2022) wakati alipofika katika kijiji hicho na kukutana na Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji iliyoundwa baada ya kukamilika kwa mradi wa kisima cha maji kwa ajili ya mifugo na matumizi ya binadamu.
Bw. Bura ameitaka kamati hiyo kushirikiana na wanakijiji kutunza miundombinu ya mradi huo na kujiwekea utaratibu wa namna ya kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na kuwepo namna wanakijiji wanavyoweza kuchangia fedha kwa ajili ya huduma ya maji ili fedha hizo zitumike kufanya matengenzo yatakayokuwa yakihitajika pamoja na matumizi mengine.
Amesema lengo kubwa la mradi huo ni kutatua changamoto ya maji na malisho na kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hususan wakulima.
Aidha, amewaeleza wanakijiji hao kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa bajeti kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa mawili katika kijiji hicho cha Matanzi ambapo kila shamba litakuwa na hekari tano ili wafugaji waweze kupata elimu ya namna ya kulima malisho ya mifugo yao.
Amewataka kuupokea mradi huo ili uwe chachu kwa wao kujifunza namna ya kulima malisho ya mifugo yao na kuondokana na adha ya ukosefu wa malisho nyakati za kiangazi.
Kwa upande Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Israel Kilonzo ameitaka Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha Kijiji cha Matanzi kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo ili mradi huo ambao wizara imejenga kwa thamani ya Shilingi Milioni 162 unakuwa na tija na kuwataka kuwa na vikao vya mara kwa mara vya namna bora ya kuendesha kisima hicho.
Amefafanua kuwa njia pekee ambayo kamati inapaswa kufanya ni kuhakikisha inatimiza majukumu yake kadri wajumbe watakavyokubaliana na kufanya matengenezo kadri yatakavyokuwa yakihitajika ili miundombinu ya mradi hupo idumu kwa muda mrefu.
Nao baadhi ya wanakijiji waliohudhuria mafunzo ya namna bora ya kuendesha mradi wa kisima hicho wameishukuru serikali kwa kuwa wamekuwa wakipata shida ya ukosefu wa maji kwa ajili ya mifugo yao nyakati za kiangazi.
Wamesema watahakikisha wanautunza mradi huo na kujiwekea utaratibu ambao utakuwa rafiki kwao na kwamba wako tayari pia kuupokea mradi wa mashamba darasa kwa ajili ya kulima malisho ya mifugo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura akishika maji kupima kasi ya maji kutoka kwenye matanki kuingia kwenye mbauti za kunyweshea mifugo maji alipofika katika Kijiji cha Matanzi kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani wakati alipofika kukutana na Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji kisima cha kijiji hicho kilichojengwa na serikali kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji pamoja na matumizi ya binadamu. (08.09.2022)
Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura akinywa maji kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya kukinga maji ya matumizi ya binadamu wakati alipofika katika Kijiji cha Matanzi kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani kukutana na Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji hicho ili kuweka mikakati ya namna ya kukiendesha kwa tija. (08.09.2022)
Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji cha Matanzi Bw. Mashaka Mang’welo akimuelezea Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura, namna miundombinu ya kisima hicho inavyofanya kazi. Bw. Bura amefika katika kijiji hicho kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani kukutana na kamati hiyo na kujionea namna miundombinu ya kisima inavyofanya kazi. (08.09.2022)
Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura akizungumza na baadhi ya wanakijiji wa Matanzi katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani pamoja na wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji hicho, ambapo amewataka kuhakikisha wanatunza miundombinu ya kisima na kujiwekea utaratibu wa kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya kupata huduma ya maji ili fedha zitakazopatikana ziwe zinatumika kufanya matengenezo pindi inapotokea hitilafu kwenye miundombinu pamoja na matumizi mengine. (08.09.2022)
Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Israel Kilonzo akizungumza na baadhi ya wanakijiji wa Matanzi wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji hicho kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani na kuitaka kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili mradi huo ambao wizara imejenga kwa thamani ya Shilingi Milioni 162 unakuwa na tija na kuwataka kuwa na vikao vya mara kwa mara vya namna bora ya kuendesha kisima hicho. (08.09.2022)
Baadhi ya wanakijiji wa Matanzi katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji hicho wakiwa kwenye mkutano wenye lengo la kutolewa kwa elimu ya namna ya kuendesha mradi wa kisima cha maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo pamoja na matumizi ya binadamu. Elimu hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura na Afisa Mifugo Mkuu kutoka katika wizara hiyo Bw. Israel Kilonzo (08.09.2022)
Baadhi ya ng’ombe katika Kijiji cha Matanzi kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani wakinywa maji kwenye moja ya miundombinu ya mradi wa kisima cha kijiji hicho uliojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji pamoja na matumizi ya binadamu. (08.09.2022)
Mradi wa maji katika Kijiji cha Matanzi kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani uliojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa thamani ya Shilingi Milioni 162 ambapo mradi huo umekabidhiwa kwa Kamati ya Usimamizi wa Miundombinu ya Maji ya kisima cha kijiji hicho ili kujiwekea utaratibu wa namna ya kuuendesha ili uwe na tija kwa wanakijiji hao kwa kuwa umejengwa kwa ajili ya kuondoa adha ya ukosefu wa maji hususan nyakati za kiangazi ambapo mifugo imekuwa iktembezwa umbali mrefu kupata maji na kusababisha migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi wakiwemo wakulima. (08.09.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni