Nav bar

Alhamisi, 22 Septemba 2022

​ULEGA: WAFUGAJI MILIKINI ARDHI NA KUFUGA KISASA KUKUZA UCHUMI

Na. Edward Kondela


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ametoa rai kwa wafugaji nchini kununua ardhi kwa ajili ya ufugaji na kuweka miundombinu muhimu na kufuga kisasa ili kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.


Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (09.09.2022) wakati alipofika katika Shamba la Mifugo la Maloloi lililopo Kijiji cha Milama Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro ili kujionea namna mtanzania huyo mwenye asili ya kimasai alivyobadilisha ufugaji wa kiasili na kufuga kisasa, kwa kuwa na mifugo bora, maeneo ya kuhifadhia mifugo pamoja na kujenga nyumba za kisasa.


Amesema wafugaji wanatakiwa kubadilika na kuondokana na migogoro ya ardhi pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa hivyo ni muhimu kwao kuacha ufugaji wa kuhamahama badala yake wanunue ardhi na kuimiliki kisheria na kufuga mifugo ambayo wana uwezo wa kuihudumia.


“Ni muhimu sana wanunue ardhi na waimiliki kwa mujibu wa sheria, inasajiliwa kwa ajili ya ufugaji anaweka na miundombinu kama majosho na kisima kikubwa cha maji kwa ajili ya uhakika wa kupata maji muda wote, itasaidia sana kufanya sekta inakuwa na mchango mkubwa.” Amesema Mhe. Ulega


Aidha, amewataka wataalam wa sekta ya mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kufika katika Shamba la Mifugo la Maloloi kumsadia mmiliki wa shamba hilo kulisajili pamoja na kulitambua kuwa ranchi ya sekta binafsi kwa wafugaji wa asili waliobadilika.


Ameongeza kuwa kwa sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya jitihada kubwa za kufungua milango ya biashara kwenye tasnia ya nyama ambapo nchi mbalimbali zikiwemo za Saudi Arabia na Oman zinahitaji nyama kutoka Tanzania hivyo ni muhimu nchi kuwa na wafugaji wanaofuga kisasa na kuwepo na uhakika wa upatikanaji wa nyama bora.


Pia, katika kuhakikisha wafugaji wanabadilika na kufuga kisasa amesema serikali kupitia Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), katika kipindi cha muda mfupi wa miaka mitano itakuwa ikitoa elimu kwa wafugaji namna bora ya kufuga kisasa ili wafugaji wengi waanze kufuga kisasa na Tanzania kuendelea kuuza nyama nje ya nchi.


Kwa upande wake mmiliki wa Shamba la Mifugo la Maloloi Bw. Maloloi Kibangashi amesema aliamua kubadilika kwa kuacha kufuga mifugo kwa njia ya asili na kuamua kuuza mifugo hiyo na kununua ng’ombe wa kisasa wakiwemo wa nyama na maziwa ili kuacha ufugaji wa kuhamahama.


Bw. Kibangashi ametoa rai kwa wafugaji wengine kubadilika kwa kufuga kisasa na kuacha ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa ukisababisha migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima, hivyo kuuza mifugo waliyonayo na kubakiza michache ambayo wanaweza kumudu kuwa nayo na kufuga kisasa.


Naye Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Natujwa Melau amesema wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Morogoro ambazo zina wafugaji wengi, ambao wamekuwa wakihamasishwa juu ya ufugaji wa kisasa kwa kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakiingia kwenye migogoro kwa kupitisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.


Amesema ni muhimu kwa wafugaji kununua maeneo na kuacha ufugaji wa kuhamahama kwa kuwa hali hiyo itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi kwa kuwa shughuli za kilimo zimekuwa zikiongezeka katika wilaya hiyo.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wafugaji wanabadilika na kufuga kisasa ili kupata tija zaidi kwa kufuga mifugo bora inayotoa nyama na maziwa mengi pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hususan wakulima.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiwa na mmiliki wa Shamba la Mifugo la Malololi lililopo Kijiji cha Milama, Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Bw. Malololi Kibangashi, ambapo Naibu Waziri Ulega amewataka wafugaji nchini kununua maeneo na kuyasajili kisheria na kuyawekea miundombinu muhimu yakiwemo majosho na visima vya maji ili kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji wa kuhamahama. (09.09.2022)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akikagua ubora wa mbuzi wa kisasa katika Shamba la Mifugo la Maloloi lililopo Kijiji cha Milama, Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, mara baada ya kufika katika shamba hilo na kuhamasisha wafugaji kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo michache na yenye tija kwa kuwa Tanzania inazidi kufungua masoko ya nyama nje ya nchi. (09.09.2022)

Muonekano wa Shamba la Mifugo la Maloloi lililopo Kijiji cha Milama, Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, ambapo mmiliki wa shamba hilo Bw. Maloloi Kibangashi mwenye asili ya kimasai amenunua eneo hilo na kujenga nyumba za kisasa na kutenga maeneo kwa ajili ya kuhifadhia mifugo, ambapo amewaasa wafugaji wenzake kubadilika na kufuga kisasa kwa kuhakikisha wananunua maeneo na kuyamiliki kisheria na kuachana na ufugaji wa kuhamahama. (09.09.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni