Nav bar

Alhamisi, 22 Septemba 2022

NARCO KUAJIRI WATUMISHI 64

Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imepata kibali cha kuajiri watumishi 64 ambao watakwenda kusimamia ranchi mbalimbali hapa nchini.

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki leo (08.09.2022) mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kilichojadili hali ya utendaji kazi wa kampuni ya NARCO bungeni Jijini Dodoma.

 

Waziri Ndaki amesema licha ya kupatikana kwa kibali cha kuajiri watumishi hao, wameieleza kamati mpango wa mageuzi wa uendeshaji wa Ranchi za Taifa ambao unaendelea kukamilishwa na pindi utakapokamilika utawasilishwa kwenye kamati hiyo.

 

Vilevile Wizara imeieleza kamati kuhusu mpango wa kuwaajiri vijana kwenye Sekta ya Mifugo ambapo kwa kuanzia tayari vimeanzishwa vituo atamizi ambavyo vitachekua vijana 240 kwa kuanzia kwa ajili ya kuwafundisha namna bora ya unenepeshaji na ufugaji ng’ombe. Vijana hawa pindi watakapomaliza watapelekwa kwenye ranchi za taifa na kupatiwa maeneo kwa ajili ya kuanza kufuga. Lengo ni kubadilisha fikra za vijana kuhusu ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa maendeleo ya uchumi.

 

Waziri Ndaki amesema zipo fursa nyingi kwenye Ranchi za Taifa ikiwemo ya uwekezaji ambapo Wizara imeshafanya kazi kubwa ya kuitangaza kampuni hiyo ndani na nje ya nchi ambapo kampuni hiyo inayo maeneo yenye ukubwa wa takribani hekta 32,500 yanayofaa kwa ajili ya shughuli za ufugaji, ujenzi wa viwanda vya nyama na mazao ya mifugo.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Yustina Rahhi amesema kuwa NARCO inatakiwa kuhakikisha inasimamia mikataba wanayoingia na wawekezaji kwani kumekuwepo na baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakikiuka utekelezaji wa mikataba hiyo.

 

Naye Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Wizara imepanga kuongeza mifugo katika ranchi zote, kuongeza idadi ya mashamba ya malisho ikiwa ni pamoja na upandaji wa malisho mapya. Vilevile Wizara imepanga kufanya ukarabati wa miundombinu ya mifugo katika ranchi za taifa ili mifugo hiyo ifugwe kwenye mazingira salama yenye kuleta tija katika uchumi kupitia mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati Sekta ya Mifugo ilipowasilisha taarifa ya mkakati wa mabadiliko kwenye Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambapo ameelezea fursa zilizopo kupitia ranchi hizo na kwamba wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanayo fursa ya kuwekeza katika ufugaji na kilimo cha malisho. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. (08.09.2022)

Baadhi ya Viongozi kutoka Sekta ya Mifugo na Wajumbe wa Kamati wakifuatilia wasilisho la taarifa ya mkakati wa mabadiliko kwenye Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) lililowasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. (08.09.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni