Nav bar

Jumamosi, 17 Septemba 2022

SHIRIKA LA MAENDELEO LA UFARANSA KUWEKEZA NCHINI TANZANIA

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Uvuvi), Bw. Emmanuel Kayuni amesema kuwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa limejipanga kuja kuwekeza kwenye uchumi wa buluu.

 

Kayuni ameyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili maeneo ambayo Shirika la Maendeleo ya Ufaransa wanaweza kushiriki kuwekeza kwenye Sekta ya Uvuvi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Wizara uliopo kwenye jengo la NBC Benki Jijini Dodoma.

 

Shirika la Maendeleo la Ufaransa limelenga kuwekeza kwenye uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo ya bahari, uzalishaji na mnyororo mzima wa mazao ya uvuvi na usimamizi wa maarifa.

 

Wizara imeweza kuelezea vipaumbele vilivyopo kwa sasa kwenye Sekta ya Uvuvi ambapo mazungumzo hayo yalishawahi kufanyika awali, hivyo kikao hicho kililenga zaidi kuangalia utekelezaji wa mambo yaliyokubalika kwenye kikao cha kwanza.

 

Kayuni amesema kuwa Sekta ya Uvuvi itawasilisha Andiko la Mradi kwenye Shirika hilo hili baada ya kukubaliana, utekelezaji wa mradi huo uweze kuanza.

 

Mratibu wa Miradi ya Shirika la Maendeleo ya Ufaransa Nchini Tanzania, Bi. Bernadeta Ngwilizi amesema kuwa lengo la kukutana na viongozi wa Sekta ya Uvuvi ni kujua vipaumbele walivyonavyo na kujadili ni nini kifanyike ili vipaumbele hivyo viweze kutekelezeka. Lakini tayari timu ya wataalam kutoka pande zote mbili ilishakutana na kujadili maeneo ambayo wanaweza kushirikiana.

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa matarajio ni makubwa kwa kuwa serikali imekuwa ikiwekeza kwenye kuwawezesha wavuvi wadogo na akina mama, uhifadhi wa maeneo ya bahari na maji baridi ili kulinda rasilimali zilizopo na kuhakikisha kuwa kuna kuwa na uvuvi endelevu.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Uvuvi), Bw. Emmanuel Kayuni (kulia) akifungua kikao cha kujadili maeneo ambayo Shirika la Maendeleo ya Ufaransa wanaweza kushiriki kuwekeza kwenye Sekta ya Uvuvi ambapo amesema kuwa Sekta ipo tayari kushirikiana na Shirika hilo kwa malengo ya kuleta maendeleo kwa wavuvi na kuwa na uvuvi endelevu. Kikoa hicho kimefanyike kwenye ukumbi wa Wizara uliopo kwenye Jengo la NBC Benki Jijini Dodoma. (05.09.2022)


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani (Uvuvi), Prof. Mohammed Sheikh akielezea vipaumbele vilivyopo kwenye Sekta ya Uvuvi wakati wa kikao kilichojadili kuhusu maeneo ambayo Shirika la Maendeleo la Ufaransa wanaweza kushiriki kuwekeza kwenye Sekta ya Uvuvi ambacho kimefanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Jengo la NBC Benki Jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango (Uvuvi), Eliyuko Mmbaga. (05.09.2022)


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (Uvuvi), Bw. Emmanuel Kayuni (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Bi Celine Robert (wa tatu kutoka kushoto), Viongozi wa Shirika hilo na Viaongozi wa Wizara mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili kuhusu maeneo ambayo Shirika la Maendeleo la Ufaransa wanaweza kushiriki kuwekeza kwenye Sekta ya Uvuvi ambacho kimefanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo kwenye Jengo la NBC Benki Jijini Dodoma. (05.09.2022)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni