Nav bar

Jumamosi, 17 Septemba 2022

​SERA YA TAIFA YA MIFUGO YA 2006 KUBORESHWA

Wizara  ya Mifugo na Uvuvi imekutana na Sekretarieti ya Mikoa na Mamlaka ya Serikali za mitaa kwa ajili ya kufanya  mapitio na kuthibitisha Rasimu ya Sera ya Taifa ya mifugo ya mwaka 2022.


Sera hiyo inaundwa baada ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya mifugo ya  mwaka 2006 baada ya kuona changamoto zimejitokeza kiasi cha kufanya ushawishi wa  kufanya mapitio na kuwa na Sera nyingine ya mifugo kwa mwaka huu.


Kauli hiyo imetolewa Septemba 5, 2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Venance Ntiyalundura wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufungua warsha ya kupitia na kuthibitisha Rasimu ya Sera hiyo.


‘’kwa hiyo mchakato ulianza kwa kupata maoni kwa wadau mbalimbali kutoka mikoa yote nchini. Rasimu ikaandaliwa ,sasa tunakutana na  wadau kuona hiyo rasimu ya sera ya mwaka 2022 kama inaweza kukidhi mahitaji yetu leo na siku zijazo au la.’’ alisema Ntiyalundura 


Wakati huo huo alisema , wanatarajia kupata maoni hayo kutoka Sekretarieti ya mikoa na Mamlaka ya serikali za mitaa  kwani huko ndiko utekelezaji unakofanyika.


‘’Katika mkutano uliopita tulikuwa tunapata maoni ya kuboresha rasimu . Wadau hawa watakapo toa maoni kulingana na uzoefu wao wa mazingira ya utekelezaji itatusaidia zaidi kuboresha rasimu hii kabla ya kuiwasilisha  serikalini kwa ajili ya kupitishwa.’’


Kwa upande wake, Ramadhani Hatibu Mshauri wa Mifugo mkoa wa Lindi alisema, kutokana na mabadiliko ya tabianchi ,ukuaji wa watu na ukuaji wa namba ya mifugo umebadilika hivyo kuna wajibu wa kuibadilisha sera ili  kuendana na mazingira ya sasa.


‘’Ile Sera  ilikuwa ya mwaka 2006 sasa hivi tunataka kutumia Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 ambayo itakuwa inaendana na uhalisia.’’


Naye, Afisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Serengeti  mkoani Mara Rehema Koka alisema lengo kuu la rasimu ya sera hiyo ni kuondoa changamoto  mbalimbali ambazo zimejitokeza kwenye sera iliyopita.


Na changamoto zilizoko ni kama vile uzalishaji mdogo na huu unatokana na kwamba tumekuwa na mifugo mingi isiyoendana na maeneo tuliyo nayo.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Venance Ntiyalundura akiongea wa wadau wa mifugo (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 iliyofanyika  Septemba 05, 2022 Jijini Dodoma.

Kiongozi wa timu ya mapitio ya sera ya mwaka 2006 kutoka Shirika la chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) Dkt. John Laffa akiwasilisha mada kwa wadau (hawapo pichani) kwenye warsha ya   kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022, iliyofanyika kwenye ukumbi wa royal village Jijini Dodoma, Septemba 05, 2022

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) (katikati), Bw. Venance Ntiyalundura akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa royal village Jijini Dodoma Septemba 05,2022

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni