Na. Edward Kondela
Wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa zinazozidi kujitokeza kuelekea uchumi wa buluu, ikiwemo ya uzalishaji wa kiumbe kiitwacho artemia kinachoishi kwenye maji chumvi ambacho kimekuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), amebainisha hayo (31.08.2022) jijini Tanga, mara baada ya kufungua kikao cha kupokea matokeo na kuhitimisha mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD) ambapo amesema kiumbe huyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na mwananchi.
Mhe. Ulega amefafanua kuwa mradi huo wa miaka miwili kuanzia 2020 hadi 2022 unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Maseno nchini Kenya, Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi nchini Kenya (KMFRI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Chuo Kikuu cha Gothenburg nchini Sweden pamoja na wakulima wa chumvi nchini Tanzania na Kenya utakuwa na tija kwa kuwa unatoa matokeo mazuri ya biashara kwa wakazi wa Ukanda wa Bahari.
Ameongeza kuwa utafiti ambao umefanywa kupitia mradi huo umebaini kuwa artemia ambaye anaishi kwenye maji chumvi amekuwa akifanya kazi ya kusafisha chumvi hivyo kuiongezea thamani kwa kuwa na rangi nyeupe na pia ana kiwango kikubwa cha protein ambacho kinahitajika kama lishe kwa samaki hususan vifaranga vya samaki.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa APTSAD nchini Tanzania Dkt. Imani Kapinga amesema kwa sasa mradi unajikita katika kutoa hamasa kwa wananchi kuwekeza katika ufugaji wa artemia ili wazalishwe kwa wingi na kuweza kutumika katika utengenezaji wa vyakula vya samaki.
Dkt. Kapinga amesema artemia ni chanzo kingine cha protein ambayo ni muhimu katika makuzi ya samaki ambapo kwa sasa bei ya Kilogramu moja ya kiumbe hicho inauzwa dola 100 za kimarekani ambazo ni sawa na takriban Shilingi za kitanzania 230,000/=.
Nao baadhi ya wakulima wa chumvi katika Mkoa wa Tanga waliohudhuria mkutano huo wamesema, kiumbe artemia atakuwa mkombozi kwao kiuchumi na kuiomba serikali kwa kushirikiana na mradi wa APTSAD kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na kuwatafutia masoko ya uhakika ili waweze kuwa na mashamba mengi kwa ajili ya kiumbe hicho.
Wamesema uzuri wa uwekezaji wa ufugaji wa artemia ni kwamba hauna gharama kubwa na wala hauhitaji chakula cha kulisha viumbe hivyo kwa kuwa vinajitafutia chakula vyenyewe na zaidi huwa ni rafiki na maeneo yenye majangwa ya chumvi.
Naibu Waziri wa Mifugo Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (kulia) akiangalia viumbe maji aina ya artemia vilivyowekwa kwenye kifaa maalum chenye maji ya chumvi kabla ya kupokea taarifa ya matokeo ya utafiti wa kiumbe hicho na kuhitimisha mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD). Kikao hicho kimefanyika jijini Tanga. (31.08.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya matokeo ya utafiti wa viumbe maji vijulikanavyo kama artemia na kuhitimisha mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD) jijini Tanga, ambapo amesema viumbe hivyo ni muhimu katika kusafisha majangwa ya chumvi baharini na kwamba vina protein nyingi ambayo ni muhimu katika makuzi ya samaki hususan vifaranga vya samaki. (31.08.2022)
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla akimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wa kikao cha mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD) jijini Tanga, ambapo Dkt. Madalla amesema wizara imekuwa ikiweka kipaumbele katika ukuzaji viumbe maji kuelekea Uchumi wa Buluu. (31.08.2022)
Mratibu wa mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD) nchini Tanzania Dkt. Imani Kapinga akifafanua matokeo ya utafiti wa kiumbe maji aina ya artemia na kuhamasisha wakazi wa Ukanda wa Bahari kuwekeza katika kufuga viumbe hao wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya matokeo na kuhitimisha mradi wa APTSAD kilichofanyika jijini Tanga. (31.08.2022)
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) aliyekaa katikati na washiriki wa mkutano wa kupokea taarifa ya matokeo ya utafiti wa viumbe maji vijulikanavyo kama artemia na kuhitimisha mradi wa Kukuza Teknolojia ya Uzalishaji wa Artemia kwa ajili ya Maendeleo Endelevu ya Ukuzaji Viumbe Maji, Usalama wa Chakula na Ukuaji wa Kiuchumi kwa Jamii za Pwani ya Afrika Mashariki (APTSAD) jijini Tanga. Mradi huo wa miaka miwili kuanzia 2020 hadi 2022 unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Maseno nchini Kenya, Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi nchini Kenya (KMFRI), Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Chuo Kikuu cha Gothenburg nchini Sweden pamoja na wakulima wa chumvi nchini Tanzania na Kenya. (31.08.2022)
(Kutoka juu) mayai ya kiumbe maji aina artemia, picha inayofuata ni artemia wakiwa hai kwenye maji chumvi na picha ya mwisho ni artemia waliokaushwa. Bei ya Kilogramu moja ya artemia ni dola za kimarekani 100 sawa na takriban Shilingi za kitanzania 230,000/= (31.08.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni