Nav bar

Alhamisi, 1 Septemba 2022

WADAU WAKUTANA KUPITIA NA KUTHIBITISHA SERA YA TAIFA YA MIFUGO NCHINI

Wadau wa mifugo wamekutana jijini Dodoma kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 yenye lengo la kuwasaidia wafugaji kuingia  katika ufugaji wa kisasa ambao utasaidia kujiimarisha kibiashara na kuchangia uchumi wa nchi.


Akifungua warsha iliyo wakutanisha wadau hao, Agosti 31,2022 Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda amesema sera hiyo ikaonyeshe namna ya kuwasaidia wafugaji wadogo na wafugaji wa asili kufanya mabadiliko katika ufugaji wao. 


‘’ Niwaombe wakati wa kupitia sera hii tuangalie ni namna gani masuala haya yamebainishwa kwenye sera mpya.’’ amesema Nzunda


Aidha, Nzunda amesema wanahitaji watu wenye mitaji kwaajili ya kuwekeza kwenye sekta ya mifugo ili kubadilisha sekta hiyo pamoja na  wawekezaji wa ndani wenye mitaji na taasisi za fedha zilizoko nchini kusaidia wawekezaji wa ndani kujenga mwitikio na uwezo wa sekta kuweza kujitegemea.


‘’Suala la kuvutia wawekezaji kwenye sekta ya mifugo na hasa wawekezaji wa kimkakati siyo bora wawekezaji maana tumepata uzoefu huko nyuma wa  wawekezaji badala ya kuendeleza sekta wamekuja kudidimiza sekta.’’ ameongeza  Nzunda.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Venance Ntiyalundura amesema sera hiyo mpya imelenga kuleta mabadiliko na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.


‘’Toka mwaka jana tulikuwa tunakusanya maoni ya wadau kwa kuangalia sera  ya Taifa ya mwaka 2006 kuona kama inakidhi mahitaji ya sekta ya mifugo.  Kipindi chote ambacho tumekuwa tukitekeleza sera ni kweli tumepata mafanikio  ya kuongeza idadi ya mifugo lakini bahati mbaya mchango wake kwa Taifa uko chini.’’ amesema Venance


Naye, Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Bw. Moses Ole Neselle amesema tangu mwaka jana wamekuwa wakishirikiana na serikali kufanya mapito ya sera ya zamani ya mwaka 2006 ili kuja na sera mpya itakayo saidia kufanya maboresho kwenye sekta ya mifugo.


‘’ Ni namna  gani sera itaendana na mabadiliko ya dunia.  Watu wameongezeka, mifugo imeongezeka ,changamoto mpya lakini fursa ni mpya zipo nyingi . Kwa hiyo ni namna gani sekta itatusaidia kuendana na hayo yote.’’ amesema Moses


Akiongea kwa niaba ya  wafugaji, Bw. Joshua Lugaso Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) amesema sera hiyo ni dira na ufunguo wa serikali kwa ajili ya kujua mahitaji ya wafugaji .


’’ Tunaamini itakwenda kuwa sera  nzuri kwa miaka yote 10 kwa ajili ya kukuza sekta ya mifugo. Tunaamini itatusaidia basi changamoto itakayo kuwepo tutajua baadae kabla sera haijapita.’’ amesema Joshua


Sera mpya itasaidia kuendeleza sekta ya mifugo itakayokuwa na mwelekeo wa kibiashara na itakayohimili ushindani wa kimataifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (kushoto) akiteta jambo na  mwakilishi kutoka Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bw.Moses Ole Neselle (kulia) mara baada ya ufunguzi wa warsha ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 kwenye ukumbi wa Dodoma hotel Agosti 31, 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akiongea na wadau wa Sekta ya Mifugo (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa warsha ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 yenye lengo la kuwasaidia wafugaji kuingia katika ufugaji wa kisasa ambao utawasaidia kujiimarisha kibiashara na kuchangia uchumi wa nchi. Agosti 31, 2022 Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Venance Ntiyalundura akiongea na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa warsha ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 na kuwasihi wafugaji kuacha kufuga kwa mazoeya na waanze kufuga kisasa na kupata tija zaidi, Agosti 31, 2022 Jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa warsha ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa warsha ya kupitia na kuthibitisha rasimu ya sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2022 mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma hotel Agosti 31,2022

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni