Shirika la kimataifa la misaada kutoka kwa watu wa Marekani (USAID) linatarajia kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa upande wa sekta ya Mifugo ili kuboresha miundombinu ya maeneo mbalimbali yaliyopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mifugo.
Hayo yamesemwa leo (17.08.2022) na Mwakilishi wa Katibu Mkuu sekta ya Mifugo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (Mifugo) Dkt. Charles Mhina mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojumuisha pande hizo mbili kilichofanyika makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
“Moja ya maeneo ambayo tumeyaangalia ni eneo la uhifadhi wa vyakula vyenye asili ya maji au “cold chain” ambapo hapa tumeangalia namna ya kushirikiana kuweza kuhifadhi maziwa hayo na kuhakikisha yanafika salama kiwandani” Ameongeza Dkt. Mhina.
Dkt, Mhina ametaja eneo jingine wanalotarajia kushirikiana na Shirika hilo kuwa ni la vyakula vya mifugo hususani kuku ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo inatokana na tafiti za hivi karibuni zilizobaini kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa kuku kutokana na kupanda kwa gharama za vyakula vya kuku ambavyo vingi huagizwa kutoka nje ya nchi.
“Na kwenye eneo hilo tumezungumzia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuzivutia sekta binafsi kujiingiza kwenye uzalishaji wa vyakula hivyo kama vile ufugaji wa nzi maarufu kama “soldier fly” ambao hutumika kutengenezea vyakula vya kuku na hapo tumeangalia namna tunavyoweza kuhamasisha matumizi ya teknolojia hiyo ili wafugaji wengi zaidi waweze kuitumia na kupunguza gharama za malisho” Ameongeza Dkt. Mhina.
Kuhusu eneo la kukabilianana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi kwa upande wa Mifugo, Dkt. Mhina amesema kuwa wamekubaliana kuongeza nguvu kwenye utoaji wa elimu ya kupanda na kuhifadhi malisho wakati wa upatikanaji wa maji ya kutosha ambapo ameongeza kuwa wanatarajia kuongeza wigo mpana wa uzalishaji wa malisho hayo kwa kuhamasisha sekta binafsi ili ziingie kwenye biashara ya uzalishaji na uuzaji wa malisho hayo.
Kwa upande wake Afisa wa Shirika la USAID anayeshughulika na Usalama wa chakula Bi. Tor Edwards amesema kuwa moja ya malengo makubwa ya Shirika hilo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula cha kutosha wakati wote hivyo anaamini kwa kuiongezea nguvu sekta ya Mifugo nchini wananchi watapata fursa ya kuwa na uhakika na upatikanaji wa mazao yatokanayo na sekta hiyo.
Ushirikiano baina ya pande hizo mbili unatarajiwa kutekelezwa kupitia awamu ya pili ya mradi wa “feed the future” ambao unalenga kuboresha mazingira ya kuhakikisha kunawepo na uzalishaji endelevu wa mazao yatokanayo na sekta ya Mifugo.
Afisa kutoka Shirika la kimataifa la misaada kutoka kwa watu wa Marekani (USAID) Bi. Tor Edwards (kulia) akielezea namna shirika hilo linavyotarajia kushirikiana na sekta ya Mifugo nchini wakati wa kikao baina yake na Menejimenti ya sekta hiyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) kilichofanyika leo (17.08.2022) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma. Kushoto ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu (Mifugo) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (Mifugo) Dkt. Charles Mhina.
Sehemu ya Menejimenti ya sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) wakimsikiliza Afisa kutoka Shirika la kimataifa la misaada kutoka kwa watu wa Marekani (USAID) Bi. Tor Edwards (hayupo pichani) wakati akielezea namna shirika hilo linavyotarajia kushirikiana na sekta ya Mifugo nchini wakati wa kikao baina yake na Menejimenti hiyo kilichofanyika leo (17.08.2022) makao makuu ya Wizara hiyo yaliyopo eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni