Nav bar

Ijumaa, 26 Agosti 2022

​RAIS SAMIA APELEKA UCHUMI WA BULUU ZIWA VIKTORIA

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni  20 kwa ajili ya kuwezesha vijana kufugaji samaki ili wanufaike na uchumi wa buluu uliopo kwenye ukanda wa Ziwa Viktoria.


Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Buchosa, Mkoani Mwanza Agosti 17, 2022.


Akiongea na vijana ambao wamepata mafunzo ya ufugaji samaki katika vizimba alisema  fedha hizo zilizotolewa na Mhe. Rais  ni fursa kubwa kwa vijana kujipatia ajira na kuondokana na kutegemea uvuvi wa asili.


"Vijana tujipange na tuchangamkie hii fursa ya kufuga samaki ili tuondokane na tatizo la ajira, tuzalishe samaki kwa wingi ili chakula kiongezeke na tuuze nje ya nchi pia," alisema


"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutoa bilioni 20 kuwawezesha  watanzania hususan vijana kufuga samaki katika vizimba katika Ziwa Viktoria", aliongeza


Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alisema mwaka huu pia Serikali itawakopesha wavuvi nchini kote boti za kisasa zaidi ya 150 ili wavuvi waweze kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wa samaki.


Aliongeza kwa kusema kuwa boti hizo zitafungamanishwa na teknolojia za kisasa zitakazomsaidia mvuvi kurahisisha shughuli za uvuvi.


Waziri Ulega aliendelea kufafanua kuwa Mhe. Rais Samia anataka kuwatoa wavuvi katika uvuvi wa kuwinda na kufanya ufugaji wa kisasa wa uhakika.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa ndani ya boti wakati akikagua eneo lililobainishwa kwa ajili ya kuweka vizimba vya kufugia samaki lililopo Wilayani Buchosa, mkoani Mwanza Agosti 17, 2022.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikagua eneo lililobainishwa kwa ajili ya kuweka vizimba vya kufugia samaki ndani ya Ziwa Viktoria lililopo Wilayani Buchosa, Mkoani Mwanza Agosti 17, 2022.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Vijana waliolengwa kunufaika na mradi wa ufugaji wa samaki kwenye vizimba alipokutana nao Wilayani Buchosa, mkoani Mwanza Agosti 17, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni