Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Mashauri ndaki amesema serikali chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuongeza bajeti ili kuziwezesha sekta za uzalishaji hususani Kilimo na Mifugo, kwa lengo la kuzalisha kwa tija na kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.
Waziri Ndaki ametoa kauli hiyo (17.08.2022) akiwa katika ziara yake ya siku moja katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), akiongozwa na mwenyeji wake Makamu mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda akiwa ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji na Ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Karimuribo.
“Kwahiyo tuwaambie vijana wenzetu kwamba kuna fursa hapa na Serikali imedhamiria kuinua sekta hizi, mwaka huu bajet imeongezeka tunaamini na mwakani zitaongezeka Zaidi kwa sababu huko ndiko watanzania wengi wanapata kipato chao.” Amesema Mhe. Ndaki
Amesema wizara yake inatarajia kuanzisha Kituo Atamizi cha Mifugo mwaka huu wa 2022 na wataalamu tayari wameanza kujifunza kupitia SUA na Kituo Atamizi (The Private Agricultural Sector Support) PASS.
“Sisi tutaenda kufanya ya mifugo lakini tunataka kujifunza kupitia hapa lakini kutokana na manufaa ambayo tunayaona na yale ambayo tunayatarajia kutoka kwenye vituo hivi inawezekana kabisa kuanzia mwakani tutaongeza bajeti na fedha kwa vituo atamizi vya kilimo, mifugo na hata kwenye uvuvi” Ameongeza Mhe. Ndaki
Aidha, ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za kilimo kwa kujiunga na vituo atamizi na kuahidi kuwa serikali ipo tayari kuwaunganisha vijana hao na taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo Kilimo (TADB) kwa ajili ya kupata mikopo.
Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda ameeleza kuwa dhamira ya chuo hicho ni kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi sanjari na kuwawezesha vijana kwa kuwapa elimu ya kilimo ili kuzalisha kwa tija na kibiashara.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambapo amesema serikali imedhamiria kuziwezesha sekta za uzalishaji hususan kilimo na mifugo ili kuongeza ajira nchini. (17.08.2022)
Baadhi ya vijana wanaosoma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) walioshiriki ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alipofika katika chuo hicho na kuelezea dhamira ya wizara kujenga Kituo cha Atamizi cha Mifugo kwa mwaka wa fedha 2022/23. (17.08.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kushoto) akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kutembelea vituo mbalimbali. (17.08.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni