Nav bar

Jumatano, 3 Agosti 2022

​DKT. MPANGO ATAKA VYOMBO VYA HABARI KUSAMBAZA ELIMU YA UFUGAJI BORA

Na. Edward Kondela


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amevitaka vyombo vya habari nchini kusambaza elimu juu ya ufugaji bora wenye tija kwa wafugaji ili kujikwamua kiuchumi.


Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo (01.08.2022) jijini Mbeya wakati akifungua rasmi Maonesho ya Wakulima Kitaifa (Nanenane) kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale, ambapo amesema ni wakati ambapo vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kujikita zaidi katika kutoa taarifa juu ya elimu ya ufugaji bora pamoja na wataalamu kutembelea wafugaji.


“Lazima tuwe na vipindi vya elimu kwa ajili ya wakulima na wafugaji wa aina zote ili wananchi waelewe namna ya ufugaji bora na faida nyingi wazipatazo.” Amesema Mhe. Dkt. Mpango


Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango akizungumza zaidi wakati akitembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye ufunguzi rasmi wa Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa mwaka 2022 yenye kauli mbiu, Kilimo ni Biashara, Shiriki, Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ametaka maboresho makubwa katika Sekta za Mifugo na Uvuvi na kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa karibu zaidi na wafugaji katika kuwapatia elimu katika tasnia hizo.


Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amemuhakikishia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kwamba wizara inajikita zaidi katika kuhakikisha inazidi kuboreshwa na kutolewa elimu zaidi kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi ili kuongeza tija katika sekta hizo ikiwemo ya uzalishaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo na ukuzaji wa wingi wa vifaranga vya samaki.


Waziri Ndaki amesema wizara imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inaboresha sekta za mifugo na uvuvi na kwamba iko kwenye mipango ya kuanzisha mashamba darasa ya malisho bora ya mifugo katika halmashauri zote nchini ili wananchi waweze kujifunza na kuwa na mashamba bora ya malisho ya mifugo.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amemuarifu Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango kuwa tayari bandari ya uvuvi inayojengwa katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ipo katika hatua za awali kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo ambao utaimarisha Sekta ya Uvuvi.


Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa Wizara inaweka kipaumbele katika kuhakikisha inaweka mkazo zaidi kwenye uchumi wa buluu ili nchi iweze kunufaika zaidi na mazao ya uvuvi kutoka bahari kuu.   


Baadhi ya wadau wa sekta za mifugo na uvuvi walioshiriki katika ufunguzi rasmi wa maonesho hayo wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa juhudi mbalimbali za kuhakikisha sekta hizo mbili zinakuwa huku wakiiomba serikali kuongeza wigo zaidi wa wataalam wa sekta hizo kuwatembelea wadau wake kwa ajili ya kuwapatia elimu.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika banda la Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kupokelewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah kabla ya kufungua rasmi maonesho hayo. (01.08.2022)


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh (kushoto) akimuelezea Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango namna idara hiyo inavyosimamia Sekta ya Uvuvi ambapo Dkt. Mpango ametaka uwekezaji zaidi katika ukanda wa Bahari ya Hindi. Makamu wa Rais ametembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kufungua rasmi maonesho hayo. (01.08.2022)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wataalamu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) wakati alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kufungua rasmi maonesho hayo, pembeni yake kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah. (01.08.2022)


Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani wa Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Anthony Dadu (wa tatu kutoka kushoto), akimuonesha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango chakula cha samaki na kumuelezea mipango ya wizara kuhakikisha upatikanaji wa wingi wa chakula cha samaki ili kuwapunguzia gharama wafugaji. Mhe. Dkt. Mpango amefika katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kufungua rasmi maonesho hayo. Kushoto kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah. (01.08.2022)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati alipomtembelea mmoja wa wadau wa Sekta ya Mifugo katika banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kufungua rasmi maonesho hayo, ambapo amefurahishwa na uwepo wa mifugo bora huku akihamasisha wafugaji kuitikia wito wa uwekaji wa hereni za kieletroniki kwa mifugo ili kutoharibu ngozi za mifugo yao. Kushoto kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb. (01.08.2022)


Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Gabriel Bura akiwa ameshika malisho ya mifugo aina ya JUNCAO na kumuelezea Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango umuhimu wa malisho hayo kwa mifugo wakati Makamu wa Rais alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) kitaifa kwa Mwaka 2022 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kufungua rasmi maonesho hayo. Pembeni ya Makamu wa Rais ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb). (01.08.2022)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni