Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha kuwa hivi sasa Wizara yake inaendelea kushauri zao la maziwa liwe zao la kimkakati ili kuifanya tasnia hiyo kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa kwa ujumla na kuboresha afya za Watanzania kwa kuondoa tatizo la udumavu nchini.
Mhe. Ulega amesema hayo kwenye kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa wakati wa hotuba yake ya kufunga maadhimisho hayo leo (01.06.2022) mkoani humo.
"Lengo letu la kufanya hivi ni kuvuta uwekezaji zaidi na umakini zaidi na hatimaye kuleta faida kwa wafugaji na taifa kwa ujumla kwa sababu pia tunatambua linagusa watu wengi wa chini hususan wanawake na vijana" Ameongeza Mhe. Ulega.
Mhe. Ulega amesema kuwa kwa sasa tasnia hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa mfugaji mmoja mmoja na inachangia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira kwa wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo hivyo ni lazima wafugaji na wote waliopo kwenye mnyororo huo waanze kujiandaa kimkakati kuhakikisha wananufaika ipasavyo pindi zao hilo litakapotangazwa kuwa moja ya mazao ya kimkakati.
Mhe. Ulega ameahidi kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Katavi kushughulikia changamoto zote zinazovikabili vikundi vya Ushirika wa wafugaji mkoani humo ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa hiyo.
"Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji wa mkoa huu ikiwa ni pamoja na zaidi ya shilingi mil.120 ambazo zitajenga kituo kikubwa cha kukusanyia maziwa mkoani hapa hivyo ni lazima tumalize changamoto hizi za ushirika ili wanufaike na fursa hizi tutakazozileta mkoani kwao" Amesema Ulega.
Mhe. Ulega amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutenga fedha za mapato yanayotokana na biashara za mifugo ili zitumike kuwawezesha wadau wa tasnia ya maziwa nchini.
"Hata kama fedha hizo zinapelekwa kwa ajili ya kununua bodaboda ambazo zitawasaidia wafugaji wetu wenye uwezo wa kuwa na vikundi zaidi ya kimoja vitakavyoajiri vijana kupitia biashara ya maziwa" Amesisitiza Ulega.
Mhe. Ulega amesema kuwa fedha hizo zinapaswa kurejea kusaidia huduma mbalimbali za Mifugo kama vile ujenzi na ukarabati wa minada ya Mifugo, kununua vifaa maalum vya kubebea maziwa na kununua ng'ombe wa maziwa.
Akizungumzia kiwango cha unywaji wa maziwa katika mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amebainisha kuwa bado kiwango hicho kipo chini ambapo kwa wastani wananchi wa mkoa huo wanakunywa lita 40 tu kwa mwaka hivyo wanaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kiwango hicho kinaongezeka.
"Maadhimisho haya yametupa manufaa mengi ikiwa ni pamoja na elimu juu ya ufugaji bora, namna ya kufanya biashara ya maziwa, vyombo mbalimbali vinavyotumika kutunzia maziwa na uwezeshwaji wa vikundi mbalimbali vya ushirika ambavyo ndio msingi mkuu wa maendeleo ya wafugaji na wengine wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa ya maziwa" Ameongeza Mhe. Mrindoko.
Mhe. Mrindoko amesema kuwa mkoa wake unaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Tasnia ya maziwa ambapo mbali na ujenzi wa kiwanda cha kati kilichopo kwenye hatua za mwisho kukamilika, Ofisi yake inawakaribisha wawekezaji mbalimbali nchini kwenda kuwekeza mkoani humo.
"Hivi sasa Mkoa wetu umefunguka na unafikika kwa njia zote ikiwa ni barabara, reli, bandari inayokaribia kukamilika na uwanja wa ndege ambao ndege kubwa zimeshaanza kutua hapo" Amesema Mrindoko.
Akitoa tathmini ya hali ya unywaji wa maziwa tangu kuanza kwa maadhimisho hayo, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya amesema kuwa takribani watu 3500 wamekunywa maziwa tangu maadhimisho hayo yalipoanza mkoani humo.
"Mhe. Naibu Waziri pia tumegawa maziwa katika maeneo mbalimbali yenye mahitaji maalum ambayo ni Shule ya Msingi Azimio, Vituo vya afya vya Ilembo na Mwangaza na kitup cha kulea watoto yatima cha Mt. Paul II" Amesema Dkt. Msalya.
Dkt. Msalya amebainisha kuwa Bodi yake ilichagua kufanya maadhimisho hayo mkoani Katavi kutokana na wingi wa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa waliopo mkoani humo hivyo walilenga kuhamasisha matumizi na usindikaji wa bidhaa hiyo jambo ambalo awali lilionekana kuwa chini.
"Na katika kutekeleza azma hiyo kwa kuanzia tumetoa jumla ya vifaa maalum kwa ajili ya kuhifadhia maziwa (CAN) 14 ambazo wazalishaji wa maziwa wa mkoa huu watazitumia kuongeza thamani ya bidhaa hiyo" Amesema Dkt. Msalya.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akimkabidhi zawadi ya maziwa na pesa taslimu mmoja wa wanafunzi waliojibu vizuri maswali yanayohusu uwekezaji wa Tasnia maziwa mkoani Katavi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa leo (01.06.2022).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni