Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara yake itashirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia tasnia ya ngozi ili kuongeza idadi ya wataalam wanaoweza kuchakata bidhaa hiyo.
Prof. Mkenda amesema hayo leo (13.06.2022) muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) lililopo kwenye maonesho ya Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET) yanayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo mbali na kuvutiwa na kazi inayofanywa na Taasisi hiyo kwa ujumla amebainisha kuwa moja ya kazi kubwa za Wizara yake ni kutengeneza wataalam wengi zaidi wanaoweza kujiajiri kupitia fani mbalimbali hivyo kinachofanywa na LITA ni kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa jukumu hilo.
“Tunayo kampasi yetu ya DIT kule Mwanza ambayo moja ya kazi yao ni kuchakata zao la Ngozi hivyo naomba muendelee kushirikiana nayo kwa ukaribu ili wote kwa pamoja tutimize lengo la Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye amelenga kuwahudumia wananchi kupitia kwetu” Amesema Prof.Mkenda.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa anaamini ushirikiano kati ya Wizara hizo mbili utasaidia kupunguza changamoto ya ajira hapa nchini kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi hizo ambapo amewataka wataalam wa pande zote mbili kukutana mara kwa mara ili kujadili mabadiliko ya teknolojia na kuzifanya taasisi hizo kwenda na wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utafiti na huduma za ushauri kutoka LITA, Joseph Msemwa amemueleza Prof. Mkenda kuwa Taasisi yao ipo tayari kushirikiana na Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Teknolojia ya Dar-es-salaam tawi la Mwanza.
“Sisi tunatoa mafunzo ya teknolojia mbalimbali zinazohusu sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa vya kisasa vinavyotumika kupima damu ya mnyama na majibu yake kupatikana ndani ya muda mfupi na kwa kufanya hivyo tunaamini tutapata mazao bora ya mifugo ikiwa ni pamoja na ngozi” Ameongeza Msemwa.
Msemwa amebainisha kuwa mpaka sasa Taasisi yake inajivunia kutoa idadi kubwa ya wataalam ambapo mbali na kufanikiwa kujiajiri, wamekuwa na msaada mkubwa kwenye jamii zinazowazunguka hasa zile zinazojishughulisha na shughuli za ufugaji na uchakataji wa mazao mbalimbali ya mifugo.
Maonesho ya Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET) yamefanyika kwa muda wa siku 7 kuanzia Juni 6 – 13, 2022 huku lengo kuu likiwa ni kuonesha matokeo yanayotokana na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Taasisi za Elimu kwa vitendo nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (kulia) akioneshwa ngozi ya ng’ombe iliyochakatwa kitaalam wakati wa ziara yake kwenye banda la Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) iliyofanyika leo (13.06.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla hajafunga maonesho ya Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET) yaliyokuwa yakifanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na huduma za ushauri kutoka Wakala hiyo, Joseph Msemwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni