Nav bar

Ijumaa, 24 Juni 2022

MAAFISA UVUVI MKOANI MARA KIKAANGONI

Na Mbaraka Kambona, Mara


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi amesema uvuvi haramu unaoendelea katika Ziwa Viktoria hususan katika Mkoa wa Mara unachangiwa na baadhi ya  Maafisa Uvuvi wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wavuvi haramu kuendeleza vitendo hivyo.


Hapi aliyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliyoifanya Mkoani humo Juni 11, 2022.


Alisema kuwa wanazo taarifa za baadhi ya maafisa uvuvi ambao wanajihusisha na vitendo vya uvuvi haramu na ndio maana hata wanapoandaa operesheni hazifanikiwi kwa sababu wao ndio wamekuwa sehemu ya kuvujisha taarifa.


"Mhe. Naibu Waziri hapa ninayo majina kadhaa ambayo yamekuwa yakijirudiarudia ya maafisa wanaotuhumiwa kushiriki vitendo vya uvuvi haramu, nikuahidi kuwa tunakwenda kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kwa ushahidi wa wazi", alisema Hapi


Kufuatia tuhuma hizo, Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuhakikisha ndani ya wiki tatu anafanya ufuatiliaji na kutathmini maafisa uvuvi wanaolalamikiwa na awasilishe taarifa kwake ili aweze kuchukua hatua za kunusuru sekta ya uvuvi.


"Mhe. Naibu Waziri, namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa afanye tathmini ya haraka hapa musoma vijijini, Manispaa, Bunda na Rorya na tutafumua mtandao wote unaohusika na vitendo hivi, ndani ya wiki tatu kutoka sasa nataka niletewe taarifa na watakaobainika kwa ushahidi wa moja kwa moja tutachukua hatua kali", alisisitiza


"Yeyote tutakauemkamata hatutasita kumchukulia hatua kwa sababu anaichafua Serikali, anahujumu uchumi wa Taifa na wananchi wanaotegemea ziwa hili", aliongeza


Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa uvuvi haramu ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazalia ya samaki hivyo ni muhimu kuyalinda na kuweka mipaka inayozuia watu kuingia katika maeneo ya mazalia ya samaki.


"Mazalia ya samaki ni lazima yalindwe kwa gharama yoyote bila hivyo rasilimali za uvuvi zitakwisha na uchumi wa watu na Taifa utadidimia", alisema


Halikadhalika aliongeza kuwa uvuvi wa dagaa ambao hauzingatii taratibu na sheria zilizopo umepelekea kupungua kwa samaki aina ya sangara kwa sababu hivi sasa dagaa na sangara wachanga wanavuliwa kwa pamoja jambo ambalo halikubaliki kisheria.


"Uvuvi wa dagaa kwa kawaida unafanyika wakati wa usiku lakini siku hizi watu hawafanyi hivyo, wanavua muda wote, matokeo yake wanavua hadi sangara wachanga na kupelekea sasa samaki aina ya sangara kupungua ", alifafanua


Aidha, aliendelea kusema kuwa Serikali ipo katika mipango ya kutafuta mashine za teknolojia rahisi ya ukaushaji wa dagaa na kuwakopesha wavuvi ili waweze kukausha dagaa wao kisasa na kuwafungasha vizuri ili wauzwe nje ya nchi na kuongeza kipato chao na kukuza pato la Taifa.


Katika hatua nyingine, Mhe. Ulega alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa hatua anazokwenda kuchukua kukomesha uvuvi haramu akisema kuwa kazi hiyo anaiweza na anaamini kwa kushirikiana na wadau wengine zoezi hilo litafanikiwa.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akishauriana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi (kushoto) muda mfupi kabla ya zoezi la uzinduzi wa Katiba ya Umoja wa Wavuvi Mara na Kanda ya Ukerewe lililofanyika Mkoani Mara Juni 11, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wadau wa Uvuvi wa Mkoa wa Mara katika hafla fupi ya uzinduzi wa Katiba ya Umoja wa Wavuvi Mara na Kanda ya Ukerewe uliofanyika Mkoani Mara Juni 11, 2022.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi akiongea na Wadau wa Uvuvi wa Mkoa wa Mara katika hafla fupi ya uzinduzi wa Katiba ya Umoja wa Wavuvi Mara na Kanda ya Ukerewe uliofanyika Mkoani Mara Juni 11, 2022.

Sehemu ya Wadau wa Sekta ya Uvuvi waliohudhuria katika hafla fupi ya uzinduzi wa Katiba ya Umoja wa Wavuvi Mara na Kanda ya Ukerewe iliyofanyika Mkoani Mara Juni 11, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni