Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha neema ambazo Mkoa wa Katavi utanufaika nazo kupitia sekta ya Mifugo kufuatia fursa mbalimbali za uwekezaji alizoziona mkoani humo.
Mhe. Ulega amesema hayo leo (31.05.2022) katika ziara yake aliyoifanya kwa kuwatembelea baadhi ya wafugaji waliopo Wilayani Mpanda ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa yanayofanyika mkoani Katavi.
“Kwa kuanzia tumefanya utaratibu wapate elimu ya ufugaji wa kibiashara lakini pia tumewaunganisha na wadau muhimu katika sekta ya ufugaji wa kisasa na kwa msingi huo na tayari kuna vifaa kadhaa vimeshatolewa na wadau hao ikiwemo mashine maalum ya kukata malisho ya ng’ombe ili iwasaidie ng’ombe hao kula chakula kwa urahisi na hivyo kutoa maziwa ya kutosha” Amesema Mhe. Ulega.
Mbali na mashine hiyo Mhe. Ulega ameongeza kuwa ili kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kuinua Sekta ya Mifugo, Wizara yake inakusudia kutumia fursa ya upatikanaji wa mazao ya mahindi na soya mkoani humo kutengeneza vyakula vya mifugo ambapo amemshauri Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mwanamvua Mrindoko kuanza kufikiria namna watakavyojipanga kuanza kunufaika na fursa hiyo kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa soya.
“Na hili sina wasiwasi nalo kwa sababu najua watu wa mkoa huu wa Katavi ni wakulima wakubwa kabisa kwa asili yao na jambo hili litahamasisha hata uwekezaji kwa sababu bado tuna uhitaji mkubwa sana wa vyakula vya Mifugo kama ng’ombe, kuku na hata samaki wanaofugwa” Amesema Ulega.
Mhe. Ulega amemuagiza Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya kushirikiana na uongozi wa mkoa huo ili kushughulikia changamoto zinazoukabili ushirika wa wafugaji wa Kashaulili ambapo amebainisha kuwa Ushirika huo ndio utakaowakomboa wafugaji waliopo mkoani humo kupitia fursa mbalimbali zitakazoletwa na wadau wa maendeleo ya sekta ya Mifugo.
“Mara baada ya kufungwa kwa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji maziwa, nakuagiza Msajili wa Bodi ya Maziwa ubaki hapa mkoani Katavi ili ushirikiane na viongozi wa Mkoa huu kupata suluhisho la changamoto zinazoukabili ushirika huu kwa sababu ninatambua wana nia ya kufanya mambo makubwa kwenye sekta hii ya ufugaji” Amesema Ulega.
Kwa upande wake Mkurugenzi mradi mkaazi kutoka Shirika la kimataifa la Heifer, Mark Tsoxo amesema kuwa Shirika lake lipo tayari kufanya kazi katika mkoa wa Katavi ambapo amesema kuwa timu yake itabaki mkoani humo kwa ajili ya kuangalia namna watakavyoweza kutekeleza shughuli zao.
“Kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na wafugaji wa Mkoa huu, tutatoa mashine kubwa ya kukatia malisho ya mifugo yenye thamani ya shilingi milioni 4 ambayo tutakukabidhi Mhe. Waziri ili ukikabidhi kikundi cha Ushirika iweze kuwasaidia kwenye shughuli zao za ufugaji” Amesema Tsoxo.
Mbali na mashine hiyo, Tsoxo ameahidi kutoa vifaa maalum vya kubebea maziwa maarufu kama “Can” kwa wafugaji waliotembelewa leo na kikundi cha Ushirika ili viwasaidie kuongeza thamani ya maziwa wanayozalisha kwa kulinda ubora wake.
Ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi imefanyika ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa yanayotarajiwa kufungwa Juni 1, 2022.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa kwenye pikipiki inayoonesha namna sahihi ya uhifadhi wa maziwa yakiwa yanasafirishwa kwa pikipiki, muda mfupi leo (31.05.2022) baada ya kufika kwenye banda la Shirika la kimaitaifa la Heifer lililopo kwenye Uwanja wa Azimio, mkoani Katavi kunakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa, anayeshuhudia kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rodrick Mpogole.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiangalia ng’ombe wanaofugwa na Bi. Anastazia Chacha (kushoto) wakati wa ziara yake ya kutembelea baadhi ya wafugaji waliopo mkoani Katavi leo (31.05.2022) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa yanayofanyika mkoani humo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni