Na. Edward Kondela
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikishirikiana na taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA) inaendelea na zoezi la utoaji wa mafunzo ya mfumo mpya wa kieletroniki wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirishia mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi uitwao Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS).
Akifungua mafunzo hayo leo (31.05.2022) kwa Kanda ya Arusha, Afisa Mifugo Mkoa wa Arusha Bi. Winfrida Joseph amewaasa wataalam wa idara na vituo vya Sekta ya Mifugo vilivyopo katika kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha, kuwa na mpango mkakati na kutumiwa vyema mfumo katika kukuza Sekta ya Mifugo nchini na kuhakikisha pia washiriki wa mafunzo wanakuwa chachu ya kwenda kuwafundisha wadau wengine wa sekta hiyo ili kutumia vyema mfumo huo.
Bi. Joseph amesema anaamini mfumo huo ukitumika vyema utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza Sekta ya Mifugo na kutumia njia ya kisasa katika biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi kwa kuwa ni mfumo ambao wa kipekee na unatumiwa kwa njia ya simu janja na kompyuta ili kupata vibali mbalimbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo Bw. Baltazar Kibola akiuelezea mfumo huo amesema unagusa maeneo yote yanayohusu Sekta ya Mifugo.
Ameongeza kuwa mfumo huo wa kieletroniki utatumika kote nchini kupitia kanda nane, na utatumika pia na taasisi zote za Sekta ya Mifugo zilizo chini ya wizara, kwenye minada pamoja na vituo vilivyo chini ya mikoa na halmashauri ambapo utawezesha kutoa vibali vya kusafirishia mifugo na mazao yake vikiwemo vyakula vya mifugo.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA) pamoja Kampuni ya ICTPACK inaendesha mafunzo ya siku tatu katika Kanda ya Arusha, juu ya mfumo wa kieletroniki ili vibali mbalimbali vya kusafirishia mifugo na mazao yake vianze kutolewa kwa njia ya kieletroniki kwa kutoa elimu kwa wataalam wa idara na vituo vya Sekta ya Mifugo.
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo Bw. Baltazar Kibola akiuelezea mfumo mpya wa kieletroniki wa usimamizi wa utoaji vibali mbalimbali vya kusafirishia mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi uitwao Mifugo Integrated Management Information System (MIMIS).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni