Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewataka wafugaji nchini kutumia vizuri fursa ya utambuzi wa mifugo kwa njia ya kielektroniki ili iweze kuwasaidia kupata bima ya mifugo yao ambayo wanaitegemea katika kukuza uchumi wao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za ukaguzi na Ustawi wa Wanyama Dkt. Annette Kitambi wakati wa ufunguzi wa utoaji mafunzo ya utambuzi wa mifugo kwa kuweka hereni za kielektroniki Disemba 20,2021 mkoani Tanga.
Alisema kuwa baada ya kusajili mifugo kwa njia hiyo mfugaji atapata fursa ya kuweka bima kwa mifugo yake ambayo anaitegemea ambapo itamsaidia kupunguza gharama za matibabu pindi mifugo itakapo kumbwa na magonjwa mbalimbali.
"Mfugaji anaweza akachagua mifugo yake ile iliyobora ambayo ataona akiipoteza atapata hasara kubwa kwa hiyo kwa kutumia zile namba anaweza akaweka bima kwa hiyo mifugo yake” alisema Dkt Kitambi.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine wafugaji watakaoshindwa kutekeleza zoezi la utambuzi watakosa fursa ya kuuza mifugo yao au kutoa mahari kama ilivyozoeleka kwa sababu mifugo hiyo itakuwa nje ya mfumo.
Kwa upande wake Afisa Mifugo Mkoa wa Tanga Issa Khatibu alisema kuwa changamoto kubwa ambayo ilikuwa ikiwakabili wafugaji mkoani humo ni muingiliano wa mifugo mingi kutoka nchi jirani.
Alisema muingiliano huo umekuwa ukisababisha wizi wa mifugo kuwa mkubwa kwa sababu ya mifugo kutotambuliwa hivyo wanaamini ujio wa zoezi hilo ni mkombozi kwa wafugaji wengi hasa waliopo mpakani.
“Tumekuwa na changamoto ya muingiliano wa mifugo kutoka nchi jirani ya Kenya kwa sababu tuko mpakani kwa hiyo hata mifugo ikiibiwa inakuwa ni ngumu kuipata lakini kwa mfumo huu wa kielektroniki utasaidia sana kuondoa changamoto hii inayotusumbua kwa muda mrefu sasa” alisema Khatibu.
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama Dkt.
Annette Kitambi (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa
Mifugo pamoja na maafisa TEHAMA wa Mkoa wa Tanga mara baada ya mafunzo ya
utambuzi usajili na ufuatiliaji wa Mifugo kwa njia ya kielektroniki Disemba
20,2021 Mkoani Tanga.
Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ukaguzi na Ustawi wa Wanyama, Dkt.
Annette Kitambi akiwasilisha mada wakati wa mkutano wa mwongozo wa
utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki
kwa maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo cha Habari na Mawasiliano
(TEHAMA), (hawapo pichani) kutoka Mkoa wa Tanga na wilaya zake. Disemba
20,2021.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bw. Sebastian Masanja
akifungua mkutano wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa
njia ya hereni za kieletroniki kwa maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo
cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA), (hawapo pichani). Disemba 20,202.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni