Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Dkt. Bora Haule amesema zoezi la utambuzi wa Mifugo kwa njia ya hereni za kielektroniki, litaleta faida nyingi ikiwepo kutambua Mifugo iliyopo katika Mkoa huo, kata na Vijiji.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya uhamasishaji wa zoezi la utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo kwa hereni za kielektroniki katika Mkoa wa Lindi, Disemba 20, 2021.
Dkt. Haule amesema zoezi la utambuzi wa Mifugo litasaidia kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pia kujihakikishia kupata Masoko ya Mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi.
Vilevile, kuwepo kwa biashara ya Mifugo na mazao yake inahitaji kuwepo kwa mfumo madhubuti wa utambuzi, usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo hiyo.
"Wakurugenzi na wataalam hakikisheni Elimu ya utambuzi inawafikia wafugaji ili kuweza kufanikisha zoezi hili kwa haraka na ufanisi zaidi".Amesema Dkt. Haule.
Aliongezea kwa kusema Wizara ya Mifugo na uvuvi imejipanga kwa kuanza na utambuzi kwa aina nne za Mifugo ikiwa ni Ng'ombe, Punda, Kondoo na Mbuzi.
Pia zoezi la utambuzi litafanyika kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapa kazi makampuni binafsi yaliyosajiliwa, na Halmashauri kuweza kununua hereni za kufanya utambuzi kwa kutumia wataalamu wake.
"Ni vizuri kila mmoja afaham vizuri miongozo, sheria na kanuni ya utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo ili waweze kutoa Elimu", Alisema Dkt. Haule.
Naye, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Dkt. Joseph Sijapenda amesema Mkoa wa Lindi unawafugaji wengi kutokana na kuwa na maeneo makubwa ya malisho, hivyo kupitia zoezi la utambuzi wa Mifugo itasaidia kutambua idadi ya Mifugo yao kwenye maeneo husika na kuweza kupata wawekezaji katika Mkoa huo.
Mgeni Rasmi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora
Haule,(katikati) akiongea na washiriki waliohudhuria kwenye mafunzo ya utambuzi
wa Mifugo kwa hereni za kielektroniki, kuhusu faida ya zoezi la utambuzi wa
Mifugo alipokuwa akifungua mafunzo hayo katika Mkoa wa Lindi, Disemba 20.2021,
(kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya jamii ya Mifugo, Dkt. Stanford
Ndibalema na (kulia) Katibu Tawala msaidizi uchumi na Uzalishaji,
Majid Myao.*
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya jamii ya Mifugo Dkt.
Stanford Ndibalema akitoa ufafanuzi wa Muongozo wa zoezi la utambuzi,
Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo kwa hereni za kielektroniki, kwenye mafunzo ya
utambuzi wa Mifugo kwa hereni za kielektroniki, mafunzo hayo yamefanyika katika
Mkoa wa Lindi, Disemba 20.2021. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni