Nav bar

Alhamisi, 13 Januari 2022

DHAMIRA YA SERIKALI NI KUWAONDOA KWENYE UVUVI WA KUWINDA-ULEGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinafanya jitihada kubwa ili kuwafanya wavuvi wawe na uhakika wa kupata samaki pindi wakienda majini badala ya kuwinda kama wanavyofanya hivi sasa.

Mhe. Ulega ameyasema hayo (21.12.2021) kwenye hafla ya kuwakabidhi wavuvi vifaa maalum  vitakavyowawezesha kutambua maeneo yenye samaki kabla ya kuingia majini na kuanza shughuli ya uvuvi iliyofanyika Shehia ya Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja (Zanzibar).

“Kwanza nimefarijika kuona wavuvi wengi kwenye shehia hii ni vijana hivyo nina uhakika itakuwa rahisi wao kutumia vifaa hivi na kuwafundisha wazee ambao bado wanaendelea na shughuli za uvuvi kwa hapa Kusini Unguja” Ameongeza Mhe. Ulega

Mhe. Ulega ameiagiza Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo ili wavuvi hao waanze kuvitumia ambapo ametoa rai kwa wavuvi kutumia vizuri teknolojia hiyo.

“ Lakini pia vifaa hivi tunavyogawa leo ni vichache hivyo niwaelekeze  mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu kuongeza wigo wa usambazaji wa vifaa hivi muhimu na hatimaye viweze kuenea kwa wavuvi wote waliopo Zanzibar na Tanzania bara” Ameagiza Mhe. Ulega.

Mhe. Ulega ameongeza kuwa hatua ya kugawa vifaa hivyo itaendelea kuchochea kampeni ya Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha pande hizo zinaingia kwenye uchumi wa buluu jambo ambalo ameweka wazi kuwa litainua uchumi wa wavuvi  kwa kiasi kikubwa.

Awali akisoma taarifa ya ulinzi wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba Kamanda wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) Comodore  Azana Msingiri amebainisha kuwa kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wavuvi kutotii sheria bila shuruti ambao huiona mamlaka yake kama kandamizi pindi wakichukuliwa hatua ambapo amewataka wavuvi kutambua kuwa ulinzi wa rasilimali za Uvuvi kwa upande wa visiwa hivyo ni jukumu ambalo mamlaka yake inalitekeleza kisheria.

“Hivi karibuni kuna tukio moja lilitokea kwa baadhi ya Wavuvi kubishana na KMKM na mimi nilipopata taarifa ya kutosha kutokana na mzozo huo niliamuru kikosi hicho kiondoke katika eneo hilo kwa sababu wangeendelea wakati wao wana silaha ingeweza kutokea hata umwagaji wa damu” Amesema Comodore Msingiri.

Comodore Msingiri amewaeleza wavuvi waliofika  kwenye halfla hiyo kuwa hakuna mtu yoyote aliyepo juu ya sheria hivyo ni vizuri kufuata maelekezo yote wanayopewa na mamlaka hiyo ambapo amesisitiza kuwa mamlaka yake imejidhatiti kuhakikisha inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Akielezea kuhusu  mapokezi ya Wavuvi kuhusu Vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa bahari Kuu Zahor El.Kharousy  amesema kuwa  tangu kuanza kutumika kwa vifaa hivyo  kiwango cha upatikanaji wa samaki kimeongezeka ambapo kwa hivi sasa mvuvi mmoja anaweza kupata kiasi cha kilo 38 za samaki kwa saa moja.

“Kuongezeka kwa kipato kinachotokana na Uvuvi kumewawezesha wavuvi hao kukidhi mahitaji yao ya kila siku na kufanya shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na baadhi yao kujenga makazi ya kudumu, kuboresha zana za Uvuvi na kusomesha watoto wao” Amesema El. Kharousy.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza jumla ya vifaa 64 vya kusomea maeneo ya upatikanaji wa samaki na simu za mkononi 21 vyote vikiwa na thamani ya milioni 200.8 viligawiwa kwa wavuvi hao ambapo amebainisha kuwa fedha zote za kugharamia vifaa hivyo zimetoka katika mradi wa SwioFish unaotekelezwa kwa ufadhili wa benki ya Dunia.

Akitoa shukran kutokana na vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Rashid Rashid amebainisha kuwa vifaa hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wavuvi waliopo kwenye mkoa wake ambapo aliwataka wavuvi hao kutumia vifaa hivyo kwa umakini ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu zaidi.

“Lakini pia nimemuomba Mhe. Ulega msaada wa majaketi ya kujiokoa na majanga ya majini ambapo ameahidi kunipatia majaketi  hayo hivyo nikushukuru sana Mhe. Ulega” Amesema Mhe. Rashid.

Mhe. Rashid ameeleza  kuwa mbali na vifaa hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu imetoa jumla ya boti 70 kwa wavuvi wote wa Mkoa wake ambapo ameongeza kuwa kinachosubiriwa hivi sasa ni kupokea boti hizo.

“Boti hizi tutazigawa kwa wavuvi na tayari wenzetu wa uvuvi wa bahari kuu wameshatupa maelekezo kuhusiana na hilo lakini vile vile Mkoa wetu umepatiwa jumla ya boti 50 za uvuvi wa mwani na muda si mrefu tutapa vifaa vya uvuvi wa kaa na majongoo hivyo tunamshukuru sana Mhe. Rais wetu wa Zanzibar  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha Uchumi wa buluu unawezekana” Amehitimisha Mhe. Rashid.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali zitakazoziwezesha nchi hizo kuingia kwenye uchumi utakaotegemea Rasilimali za Uvuvi zilizopo ukanda wa bahari kuu (Uchumi wa buluu).


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (mwenye suti nyeusi na shati jeupe katikati) akimkabidhi mmoja wa wavuvi wa Shehia ya Kizimkazi simu itakayomuwezesha kutambua mahali penye samaki wengi  baharini katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika l (21.12.2021) Mkoa wa Kusini Unguja (Zanzibar). Wengine pichani ni baadhi ya Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioshiriki tukio hilo.* 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifafanua mambo yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha pande hizo kwa pamoja zinaingia kwenye Uchumi wa buluu wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa maalum vitakavyomuonesha Mvuvi sehemu yenye samaki wengi baharini iliyofanyika  (21.12.2021) Mkoa wa Kusini Unguja (Zanzibar).

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni