Wafugaji hapa nchini wametakiwa kumiliki maeneo kwa kutumia njia halali na kuhakikisha wanayaendeleza ikiwa ni pamoja na upandaji wa malisho katika maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati alipofanya mikutano na wananchi wa
vijiji vya Kapele, Ikana, Mpapa na Samang’ombe wilayani Momba mkoani Songwe
alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi.
Waziri Ndaki amesema wafugaji
wanatakiwa kutambua kuwa wanatakiwa kumiliki maeneo kihalali kwa ajili ya
kufanyika shughuli za ufugaji kama ambavyo wakulima na watumiaji wengine wa
ardhi wanavyomiliki.
"Wafugaji mnatakiwa
kumiliki maeneo kihalali ambayo ukubwa wake utaendana na idadi ya mifugo mnayotaka
kufunga na kuhakikisha mnayatunza na kuyaendeleza," alisema Waziri Ndaki
Pia Waziri Ndaki amesema
Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji na
malisho ya Mifugo ambayo yatalindwa kisheria na kukabidhiwa kwa wafugaji. Yapo
maeneo ambayo yametengwa katika vijiji kwa ajili ya shughuli za ufugaji lakini
bado hayajakabidhiwa kwa wafugaji.
Aidha, wafugaji wameshauriwa
kuanza kuvuna mifugo yao pale wanapoona idadi ya mifugo imekuwa kubwa kuliko
eneo wanalolimiliki. Hivyo amewasihi kuanza kuvuna mifugo ili wabaki na mifugo inayoendana
na ukubwa wa maeneo wanayoyamiliki.
Vilevile amesema kuwa moja ya
sababu ya migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hasa wakulima ni
suala la malisho. Hivyo amewataka wafugaji kuanza kupanda malisho katika maeneo
watakayoyamiliki na kuacha kutegemea malisho ya asili peke yake.
Kuhusu malalamiko ya wakulima kupigwa na wafugaji, Waziri Ndaki amewataka wafugaji na wakulima kuheshimiana kila mmoja kulingana na shughuli wanazofanya kwani kwa kufanya hivyo hakutakuwa na migogoro. Lakini pia ameuagiza uongozi wa wilaya uhakikisha wanawachukulia hatua za kisheria wafugaji ambao watabainika kuwa wamewapiga wakulima.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kapele na Ikana
ambapo amewataka wananchi hao kuheshimiana kulingana na kazi wanazofanya kwani
kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa migogoro iliyopo ya wafugaji na watumiaji
wengine wa ardhi. (04.10.2021)
Mkurugenzi wa Idara ya
Uendelezaji Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Asimwe
Rwiguza akiwahamasisha wananchi (wafugaji) wa Kijiji cha Kapele kuhakikisha wanakuwa
na mashamba ya malisho ya mifugo yao lakini pia Halmashauri za Wilaya Nchini
kutenga maeneo kwa ajili kilimo cha malisho ili wafugaji waanze kujifunza na
kuanza kulima malisho katika maeneo yao. (04.10.2021)
Wananchi katika maeneo
tofauti wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati
alipofanya ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi na kutatua
kero zinazohusu sekta ya mifugo na uvuvi mkoani Songwe. (04.10.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni