Nav bar

Alhamisi, 21 Oktoba 2021

WADAU TASNIA YA MAZIWA WATAKIWA KUZINGATIA MPANGO KABAMBE WA UENDELEZAJI WA MIFUGO NCHINI

Wadau wa Tasnia ya Maziwa nchini wametakiwa kuzingatia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Miaka 5 wa  Uendelezaji wa Sekta ya Mifugo nchini ili tasnia hiyo iweze kukua vizuri na kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Wito huo ulitolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania alipokuwa akifungua Warsha ya kujadili vipaumbele vya uwekezaji katika tasnia ya maziwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo Oktoba 6, 2021.

Wakati akifungua Warsha hiyo, Zephania alisema kuwa tija itokanayo na uzalishaji wa maziwa nchini bado ndogo huku akisema kuwa uzalishaji wa maziwa kutoka katika Ng'ombe wa asili ni kati ya lita 2 hadi 1. 5 kwa siku hususan wakati wa kiangazi, kiasi ambacho ni kidogo sana.

"Natambua mwaka huu tumepanga kuhimilisha Ng'ombe Milioni 1 ili ndani ya miaka mitano ijayo tuwe na Ng'ombe waliohimilishwa wafikie Milioni 5, tunafanya hivi ili tuongeze idadi ya Ng'ombe ambao wameboreshwa ili tija ya uzalishaji wa maziwa iweze kuonekana," alisema Zephania

Aliongeza kwa kusema kuwa mpango Kabambe wa kuendeleza Sekta ya Mifugo umeainisha maeneo mbalimbali ya uzalishaji kulingana na mazingira yaliyopo ili mfugaji aweze kufanya ufugaji wenye tija.

"Maeneo yaliyoanishwa kwa ajili ya uzalishaji wa aina tofauti za  mifugo yanafahamika, maeneo hayo yamegawanywa kikanda na kila eneo lina aina ya mifugo inayoweza kustawi vizuri zaidi kuliko eneo lingine, naomba tuzingatie mpango huo uliowekwa," alisisitiza

Aidha, aliwahimiza wadau hao pia  kushirikiana vyema na Serikali katika kuwaelimisha Wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa unaozingatia mpango huo ili wajue kwa nini wafuge ng'ombe wa maziwa katika eneo fulani na kwa nini wasifuge Ng'ombe wa nyama katika eneo fulani.

Zephania aliendelea kusema kuwa Sekta ya Mifugo inahitajika kuendelea kukua ili izalishe ajira nyingi kwa vijana, waweze kujiajiri na kujikwamua kimaisha.

Pia, aliwataka wadau hao kuhamasisha unywaji wa maziwa ili kukuza soko la maziwa nchini huku akiwataka wadau wote wa uzalishaji wa maziwa watambulike ili Serikali iweze kuwashirikisha kikamilifu katika kila eneo.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania akiongea na Wadau wa Tasnia ya Maziwa katika Warsha ya kujadili Vipaumbele vya uwekezaji katika eneo hilo.


Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Amos Zephania akiongea na Wadau wa Tasnia ya Maziwa katika Warsha ya kujadili Vipaumbele vya uwekezaji katika kila eneo la tasnia hiyo ili kuongeza tija ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Miaka 5 wa Uendeleza wa Sekta ya Mifugo nchini. Warsha hiyo ya siku moja ilifanyika jijini Dodoma Oktoba 6, 2021. Katika Warsha hiyo, Zephania aliwataka wadau hao kuzingatia Mpango Kabambe huo ili mchango wa Tasnia ya Maziwa uweze kuonekana.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo), Amos Zephania ( wa pili kutoka kushoto, mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Tasnia ya Maziwa muda mfupi baada ya kufungua Warsha ya kujadili Vipaumbele vya uwekezaji katika tasnia hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini. Warsha hiyo ilifanyika jijini Dodoma Oktoba 6, 2021.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni