WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Maofisa Uvuvi kuacha kuwatoza ushuru wa kusafirishia mazao ya uvuvi nje ya nchi wafanyabiashara wa dagaa wanaofanya biashara hiyo kwa lengo la soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe.
Ametoa maagizo hayo jana (04.10.2021)
wakati akiongea na wafanyabiashara wa dagaa katika mji wa Tunduma wilayani
Momba mkoani Songwe akiwa katika ziara yake ya siku mbili, ambapo
wafanyabiashara hao wamedai kuwa wamekuwa wakitozwa ushuru huo wakati baadhi
yao hawasafirishi dagaa nje ya nchi.
Waziri Ndaki alisema
wafanyabiashara wanaopaswa kutozwa ushuru wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje
ya nchi, ni wafanyabiashara wa dagaa ambao hununua na kuuza kwenye masoko
yaliyopo nje ya Tanzania ambapo kwa Tunduma huuzwa zaidi nchi za Zambia na
Congo. Hivyo aliwataka maafisa uvuvi kuacha kuwatoza ushuru huo wafanyabiashara
wanaouza dagaa kwenye soko la ndani.
"Tuache mara moja
kuwatoza wafanyabiashara wa dagaa ambao wanauzia kwenye soko la ndani ushuru wa
kusafirishia mazao ya uvuvi nje ya nchi katika mkoa wa Songwe kwa kigezo kuwa
wote wanaziuza nje ya nchi,” alisema Waziri Ndaki
Aidha, Waaziri Ndaki aliwataka
wafanyabiashara hao kufanya biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na pia
kuacha tabia ya kutorosha dagaa kwa kutumia njia zisizo rasmi kwa lengo la
kukwepa kulipa ushuru. Vilevile aliwaeleza kuwa endapo mfanyabiashara
atakamatwa kwa kosa la utoroshaji dagaa atanyang’anywa leseni, mzigo wa dagaa
pamoja na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Awali Mbunge wa Jimbo la Momba,
Condester Sichalwe akiongea kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Ernest
Silinde ambaye hakuwepo kwenye ziara hiyo, alisema kuwa suala la wafanyabiashara
wa dagaa katika soko la ndani ya nchi kwenye mkoa wa Songwe kutozwa ushuru wa
usafirishaji mazao ya uvuvi nje ya nchini (Export Loyality) ni kero ya muda
mrefu ambayo imekuwa ikiwaumiza wafanyabiashara hao pamoja na wananchi
wanaonunua dagaa.
Shaban Ally ambaye ni mfanyabiashara
dagaa, amemshukuru Waziri kwa maamuzi aliyoyachukua ya kuondoa ushuru huo kwa
wafanyabiashara wanaouza dagaa kwenye soko la ndani kwani kilikuwa ni kilio
chao cha muda mrefu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni