Mradi wa ukarabati wa soko la kimataifa la Samaki la Feri umepangwa kutekelezwa kwa muda wa miezi saba bila kuathiri shughuli za wafanyabiashara na wavuvi.
Hayo yamesemwa leo (04.07.2021) na Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kwenye mkutano na wafanyabiashara na wavuvi wa soko
la kimataifa la samaki la feri jijini Dar es Salaam uliokuwa na lengo la
kuwaelimisha kuhusu nia ya serikali kufanya ukarabati katika soko hilo.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri Ndaki amesema kuwa
Wizara yake imeandaa mpango wa uhamishaji wa watu kwa muda katika maeneo ya
soko yatakayofanyiwa ukarabati kabla ya kuhamishiwa.
“Wafanyabiashara katika kanda 1 na 2 watatambuliwa na
kuhamishiwa maeneo ya muda yaliyoandaliwa. Mpango huu utahakikisha kuwa baada
ya ukarabati wafanyabiashara waliohamishwa watarudishwa katika maeneo yao ya
awali”. Amesema Waziri Ndaki.
"Lengo
ni kuhakikisha tunawawezesha wavuvi kuongeza ufanisi na tija katika kazi yao
sambamba na kuongeza mchango wao katika pato la Taifa, mwaka 2021 pato la Taifa
ilikuwa ni asilimia 1.7, tunakusudia siku zijazo pato hili likue" aliongeza
Waziri Ndaki.
Aidha Waziri Ndaki amesema miundombinu ya uvuvi
hususan mialo na masokoni ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mazao ya uvuvi
yanakuwa bora na salama kwa ajili ya afya ya walaji na hivyo kupata masoko ya
ndani na nje ya nchi.
Amesema miundombinu ya uvuvi inasaidia katika kudhibiti
uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi, ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya
Serikali na upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi za uvuvi.
Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega
amesema kuwa Rais Samia Hassan amejipanga kuhakikisha uzalishaji wa samaki na
mazao yake unaongezeka na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi kwenye pato
la taifa.
Naibu Waziri Ulega amesema serikali imepanga kununua meli
kubwa ambazo zitakuwa zinafanya shughuli za uvuvi kwenye bahari kuu. Pia
serikali itaweka miamba ambayo sio ya asili kwenye maeneo ya bahari ambayo
itatumika kama maeneo ya mazalia ya Samaki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anaeshuhulikia sekta ya uvuvi, Dkt.Rashid Tamatamah amesema kuwa soko hilo
limeweza kutoa ajira rasmi zipatazo 117 na ajira zisizo rasmi takribani
2,780 hata hivyo soko hilo limekuwa na watumiaji 10,000 kwa siku wakati
uwezo wa soko ni kuhudumia watu 1,500 kwa siku hivyo ni muhimu soko hilo
kukarabatiwa.
Vilevile amesema kuwa mapato yatokanayo na soko
la Feri ni kati ya Shilingi Milioni 135 hadi 150 kwa mwezi kutegemeana na hali
ya uvuvi kwa mwezi husika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakuu wa Wilaya za
Kigamboni na Ilala wamesema kuwa ukarabati wa soko hilo ni muhimu sana kwani ni
moja ya chanzo kikubwa cha mapato kwa wafanyabiashara, wavuvi na serikali.
Serikali inatarajia
kutumia kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa
mialo na masoko kwa kuweka miundombinu mbalimbali ya kuongeza thamani ya mazao
ya uvuvi na kupunguza upotevu baada ya kuvunwa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza na wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo aliwaeleza kuwa Mhe. Rais Samia Hassan amejipanga kuhakikisha uzalishaji wa Samaki na mazao yake unaongezeka na kuimarisha uchumi wa wadau wa sekta hiyo na pato la taifa kwa ujumla. (04.07.2021)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa taarifa fupi kuhusu hatua zitakazofuatwa katika ukarabati wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa miundombinu iliyopo katika soko hilo ina uwezo wa kuwahudumia watu 1,500 kwa siku lakini kwa sasa watu wanaopata huduma ni zaidi ya 10,000 hivyo ni muhimu soko hilo likarabatiwe. (04.07.2021)
Mbunge wa Jumbo la Ilala, Mhe. Mussa Zungu akizungumza kwenye Mkutano wa wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam. (04.07.2021)
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni. Mhe. Fatma Nyangasa akizungumza na wafanyabiashara na wavuvi wa soko la Kimataifa la Samaki la Feri Jijini Dar es Salaam ambapo ameahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha ukarabati huo unafanyika na kukamilika ndani ya muda uliopangwa. (04.07.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni