Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki ameumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wananchi waliovamia kwenye vitalu katika Ranchi ya Kagoma na wawekezaji ambao wanamiliki vitalu hivyo.
Waziri Ndaki ameumaliza
mgogoro huo leo (10.07.2021) baada ya kuwasikiliza wananchi na wawekezaji
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Rutoro wilayani Muleba
Mkoa wa Kagera.
Akizungimzia kuhusu mgogoro
huo, Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi kuwa maeneo hayo waliyoyavamia ni mali ya
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo tayari yalikuwa yameshakodishwa kwa
wawekezaji wanaofanya shughuli za ufugaji hivyo walipaswa kuondolewa. Lakini
kutokana na busara za Mhe. Rais Samia ameridhia eneo hilo lipimwe na wananchi
wabakizwe kwenye vijiji vinne vilivyopo ambavyo ni Kijiji cha Rutoro,
Byengeregere, Chobuheke na Mishambya vilivopo katika Kata ya Rutoro.
“Ninyi wananchi mnatakiwa
kumshukuru sana Rais Samia kwa maamuzi yake ya kuwabakiza katika maeneo haya. Lakini
niwasihi kuwa watulivu wakati wa zoezi la upimaji wa maeneo na kutoa
ushirikiano kwa wataalam watakao kuja kutekeleza zoezi hilo,” alisema Waziri
Ndaki.
Vilevile amewataka wananchi
kutoendelea kuvamia maeneo mengine katika ranchi hiyo kwani wakifanya hivyo kwa
sasa watachukuliwa hatua. Waziri Ndaki pia ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia
ya kuuza maeneo hayo wakati wao wenyewe hawajamilikishwa.
Pia kwa upande wa wawekezaji
hao amewahakikishi kuwa zoezi hilo la upimaji wa maeneo halitaathiri shughuli
zao za ufugaji kwa kuwa utawekwa utaratibu mzuri. Vilevile amewaeleza kuwa
maamuzi hayo ya kupima maeneo na kuweka alama za mipaka yatasaidia sana
kupunguza migogoro ya ardhi na kufanya pande zote kuishi kwa amani.
Katika mkutano huo yalitolewa
malalamiko kuwa wafugaji wanalisha mifugo kwenye mashamba yao na kuwasababishia
hasara. Kutokana na hilo Waziri Ndaki aliwaagiza wafugaji hao kuacha tabia hiyo
kwani ni moja ya vitu vinavyosababisha tatizo la njaa kwa wananchi na kuleta migogoro
baina ya pande zote mbili.
Vilevile wawekezaji
wametakiwa kuhakikisha wanayatumia maeneo waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa
na si vinginevyo. Aidha, uongozi wa wilaya ya Muleba umetakiwa kuweka utaratibu
utakaotumika kuwaondoa wavamizi kwenye vitalu ambao wameingiza mifugo yao
wakati hawajamilikishwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba,
Mhe. Toba Nguvila amemuhakikishia Waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watakwenda
kuyasimamia kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kagera na uongozi wa Kampuni
ya Ranchi za Taifa (NARCO).
Kutokana na uamuzi
uliochukuliwa wa kupima maeneo hayo kwenye ranchi ya Kagoma, wawekezaji na
wananchi wote wameonesha mtazamo chanya kwani hata wao wenyewe hilo ndio
wameliona ndio suluhisho.
Kata ya Rutoro yenye vijiji
vinne vya Rutoro, Byengeregere, Chobuheke na Mishambya
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wananchi na wawekezaji waliopo kwenye Ranchi ya Kagoma kuhusu mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza maeneo yaliyovamiwa na wananchi yapimwe ili wawekezaji waweze kubakiwa na eneo ambalo halitakuwa na mgogoro na kwamba baada ya kupimwa atakae vamia eneo la mtu atachukuliwa hatua. (10.07.2021)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza jambo Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora (katikati) wakati wa mkutano wa kutatua mgogoro kati ya wananchi na wawekezaji kwenye Ranchi ya Kagoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe. (10.07.2021)
Wananchi na wawekezaji katika Ranchi ya Kagoma wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi katika ranchi hiyo. (10.07.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba, Chama cha Mapinduzi na wawekezaji katika Ranchi ya Kagoma mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili hali ya migogoro kwenye Ranchi hiyo. (10.07.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni