Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki amewataka wawekezaji kwenye vitalu vya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufuata taratibu zilizowekwa kulingana na mikataba yao.
Ndaki ameyasema hayo leo
(09.07.2021) wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera wakati alipotembelea Ranchi ya
Mabale na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji wenye mifugo katika vitalu hivyo.
Waziri Ndaki amesema
kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wawekezaji kuchukua vitalu na kutovitumia kama
ilivyoelekezwa kwenye mikataba kitu ambacho kinasababisha maeneo kuwa mapori na
kuvamiwa na watumiaji wengine wa ardhi.
Wizara kupitia NARCO
imejipanga kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya vitalu kwa ajili ya kufugia
kitu ambacho kitasaidia kuondokana na tatizo la malisho na kupunguza migogoro
ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine.
“Hivyo wizara kwa sasa
imejipanga kuhakikisha wawekezaji katika vitalu wanatumia maeneo hayo kwa
malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati,”
alisema Waziri Ndaki.
Vilevile alisema kuwa wizara
kwa sasa inaiona NARCO kama ni sehemu ya kotokea kwani kupitia kampuni hiyo wizara
itaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuongeza kipato wa wafugaji.
Akiwa katika Ranchi hiyo
Waziri Ndaki amemtaka mwekezaji wa Kampuni ya Chobo Investment kuachia eneo analolimiliki
kwa sasa wakati akiendelea kujipanga ili wawekezaji wengine ambao tayari wanayo
mifugo waweze kulitumia. Aidha, amemuhakikishia mwekezaji huyo kuwa atapewa
eneo kwenye Ranchi nyingine ikiwa atafuata masharti ya mkataba wa NARCO.
Vilevile kutokana na
changamoto iliyoibuliwa kuhusu muda mfupi wa ukodishaji vitalu, Waziri Ndaki
amewaagiza NARCO kuangalia uwezekano wa kuongeza muda wa mikataba ya muda mfupi
ili iwe ni ya miaka mitano badala ya mwaka mmoja wa sasa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel
amesema wizara imejipanga kuhakisha uzalishaji wa Mifugo na mazao yake
unaongezeka na kuhakikisha wawekezaji katika sekta wanasaidiwa ili wasikwame
katika uwekezaji wao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu
wa Wilaya ya Misenyi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Abdallah Mayomba amesema
kuwa uwepo wa Ranchi katika Wilaya hiyo umesaidia sana kupunguza migogoro ya
ardhi lakini pia imesaidia kupunguza tatizo la malisho ambalo lilikuwa
linawasumbua wafugaji.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wawezekaji hao wamemueleza waziri kuwa bado wanahitaji maeneo kwa ajili
ya kufugia na kuwa wanaishukuru serikali kupitia NARCO kwa ajili ya kutenga
maeneo hayo na kuwashushi gharama ya ukodishaji wa vitalu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza na wawekezaji waliochukua vitalu katika Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera ambapo amewaagiza kuhakikisha wanayatumia maeneo hayo kwa malengo yaliyokusudiwa kwani wasipofanya hivyo watanyang’anywa na kupatiwa wawekezaji wengine. (09.07.2021)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wawekezaji katika Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera ambapo pia amewaeleza kuwa wizara inamalengo ya kuhakikisha uzalishaji wa mifugo na mazao yake unaongezeka. (09.07.2021)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiwa kwenye kitalu namba 2 kinachomilikiwa na mfugaji, Primus Karokola (kulia) wakati alipotembelea kitalu hicho kuangalia mifugo iliyopo kwenye Ranchi ya Mabale wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel. (09.07.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni