Na. Elibariki Mafole, Dodoma.
Mradi
wa uboreshaji na uendelezaji mbari za ng’ombe wa maziwa (ADGG) ambao umefanyika
katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Iringa, Mbeya Njombe, na Songwe
wawanufaisha wafugaji katika maeneo hayo.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania
(TALIRI), Prof. Erick Komba (31.05.2021) baada ya kumalizika kwa kikao cha
tathmini ya maendeleo ya mradi huo ambao kwa hapa Tanzania unafanyika katika
mikoa saba (7) na Halmashauri ishirini nan ne (24).
Prof.
Komba amesema mradi huo ulikuwa ni wa miaka sita na unatarajiwa kumalizika
mwaka 2022 mwezi wa nne. Lengo la kikao hicho cha tathmini ilikuwa ni kuangalia
mazuri yaliyofanyika kupitia mradi na namna gani yanaweza kuendelezwa ili
wafugaji waendelee kupata tija na kukuza kipato ufugaji.
“Wafugaji
wamenufaika sana kutokana na uwepo wa mradi huu kutokana na ushauri mbalimbali
waliokuwa wakiupata kutoka kwa wataalamu juu ya nini cha kufanya pale mifugo
yao inapopata matatizo na aina gani ya mbegu bora za ng’ombe wa maziwa
wanatakiwa kufuga,” alisema Prof. Kombe.
Katika
kikao hicho pia wamejadili namna ya kuwashirikisha wadau mbalimbali ambao
watasaidia kuendeleza kazi zilizofanywa na mradi ili ziwe kuwa endelevu ikiwepo
serikali, wadau wa maziwa na wadau wa mawasiliano.
Lengo
ni kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongezeka hapa nchini na hivyo kupunguza
uagizaji wa maziwa kutoka nje ya nchi na hivyo kumnufaisha mfugaji wa hapa
nchini kwa kukuza kipato chake.
Naye
Mshauri wa Mradi wa kuendeleza mbari za ng’ombe wa maziwa, Dkt. Maria Mashingo
ambaye pia alishawahi kuwa Katibu Mkuu Mifugo amesema mradi huu ni muhimu sana
katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya maziwa kwa kuhakikisha kuna kuwa na mbegu
au vizazi bora vya ng’ombe ambao wanauwezo mkubwa wa kutoa maziwa mengi.
Dkt.
Mashingo amesema mradi huu umetekelezwa kwa kutumia mbinu kubwa ambayo katika
Sekta ya Mifugo haijawahi kufanyika kwani kinachofanyika ni pamoja na utambuzi
wa ng’ombe kwa kujua uzazi na ubora wake.
Hivyo
ameshauri itafutwe njia ya kuhakikisha matokeo ya mradi huu yanaendelezwa kwani
watafiti wamefanya kazi kubwa ambayo imeleta tija kwa wafugaji kwa kuongeza
uzalishaji wa maziwa na kuongeza kipato chao.
Msimamizi
Mkuu wa Mradi wa ADGG, Dkt. Daniel Mwakihangilo amesema wamekuwa wakiwashauri
wafugaji juu ya matumizi ya mbegu bora za ng’ombe wa maziwa ikiwa ni pamoja na
matumizi ya madume bora ambayo yanapatikana katika maeneo wanayoishi na kwa
kutumia njia ya uhimilishaji ili wapate ng’ombe wenye uwezo wa kutoa maziwa
mengi.
Mratibu
wa mradi wa ADGG na Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Duniani, Dkt.
Eliamoni Lyatuu amesema kwanza walikuwa na lengo la kuwa na mfumo wa ukusanyaji
wa taarifa za mifugo, pili kuweza kurejesha mrejesho kwa wafugaji pale
wanapokuwa na maswali au maoni na tatu ni kuipanga mifugo kulingana na ubora
wake ili kuwasaidia wafugaji kupata mifugo sahihi yenye uwezo wa kutoa maziwa
mengi.
Akizungumzia
kuhusu mradi huu, Bi. Yusta Elisha ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa
amesema kupitia mradi wa ADGG wameweza kupata maelekezo juu ya ufugaji bora,
wamekuwa wakipata ujembe kupitia simu juu ya namna ya kuendeleza shughuli zao
za ufugaji ambazo zimewasaidi kuongeza uzalishaji wa maziwa tofauti na kiwango
cha maziwa walichokuwa wakikipata kipindi cha nyuma.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba akisikiliza mada iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa katika kikao kilichofanyika katika Makao Makuu ya Taasisi hiyo Jijini Dodoma. (31.05.2021)
Mratibu wa mradi wa ADGG, Dkt. Eliamoni Lyatuu akiwasilisha mada kuhusu mradi wa Uboreshaji na Uendelezaji wa Mbari za Ng'ombe wa Maziwa katika kikao kilichofanyika katika Makao Makuu ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania Jijini Dodoma. (31.05.2021)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni