Akizungumza mara baada ya
kutembelea vijiji vya Fukayosi na Mkenge vilivyopo katika wilaya hiyo na
kukagua eneo la mipaka ya vijiji hivyo na ranchi ya Ruvu inayosimamiwa na
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.
Abdallah Ulega amesema maeneo hayo yaliyotengwa watapatiwa wafugaji wenye
uhitaji kwa utaratibu maalum utakaowekwa na NARCO pamoja na serikali ya wilaya
ya Bagamoyo.
Naibu Waziri Ulega ameutaka
uongozi wa NARCO ambao umesema kuanzia Julai 15, 2020 wataanza kupokea maombi
kwa wafugaji wenye uhitaji wa vitalu katika ranchi hiyo na kutaka wafugaji
kutoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima kwa kuwa serikali inatoa maeneo
hayo ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Kuhusu uhaba wa maeneo katika
wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri Ulega amewataka watu waliopatiwa maeneo
makubwa katika wilaya hiyo kuyaendeleza, hii ni baada ya kubaini uwepo wa
maeneo makubwa katika vijiji vya wilaya hiyo ambayo hayajaendelezwa na
kuwafanya wakulima na wafugaji katika maeneo hayo kukosa sehemu ya kulima na
kufuga.
Awali wananchi hao
walimweleza Naibu Waziri Ulega kero kubwa waliyo nayo kuwa ni uhaba wa ardhi
unaopelekea wafugaji kukosa malisho na kulisha mifugo yao katika mashamba ya
wakulima na kusababisha migogoro isiyokwisha.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainab Kawawa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa wakijadili juu ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani humo mara baada ya kutembelea moja ya vijiji vinavyopakana na Ranchi ya Ruvu. (02.07.2020)
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimuelekeza Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi
za Taifa (NARCO), Bw. Masele Mipawa kuhakikisha anasimamia vyema hekta elfu 20
zinazotolewa kwenye Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya kutenga vitalu vya ufugaji na kuhakikisha
kipaumbele kiwe kwa wafugaji wanaozunguka ranchi hiyo. (02.07.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni