Serikali imesema
imedhamiria kuhakikisha wadau wa sekta ya uvuvi nchini wanapata fursa zilizopo katika
sekta hiyo kwa kutambuliwa katika mfumo ulio rasmi ili waweze kuchukua mazao ya
samaki yatakayowawezesha kuinua vipato vyao.
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo wakati akishuhudia utiaji saini kati ya
Benki ya Posta Tanzania (TPB) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania
(CHAKUWATA) na kuzindua rasmi Wavuvi Akaunti, katika mwalo wa Igombe uliopo
Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, ambapo amewataka wadau hao kuhakikisha
wanajiunga na akaunti hiyo ili waweze kupata huduma za kifedha
zitakazowawezesha zana za kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi ambazo
zitawafanya kupata malighafi kwa wingi.
“Ninawaomba wavuvi mfungue
Wavuvi Akaunti katika Benki ya Posta Tanzania (TPB) itakuwa rahisi kwenu kupata
msaada ili muweze kufanya biashara ambapo viwanda sasa vimeanza kufufuliwa
upya, nasi tumeagiza kwa sasa samaki wote wanaozalishwa katika viwanda vyetu ni
lazima wasafirishwe moja kwa moja kwenda nchi za nje kupitia viwanja vyetu vya
ndege badala ya kusafirishwa kwenda nchi zingine kupitia viwanja vya ndege vya
nchi jirani.” Amesema Mhe. Ulega
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) Bw. Sabasaba Moshingi alisema utiaji
saini kati ya benki hiyo na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania
(CHAKUWATA), ni muhimu kwa kuwa huduma ya Wavuvi Akaunti itawawezsha wavuvi
wengi kuwa na utaratibu wa
kutumia huduma za kibenki
kwa kuwa kwa sasa wengi wao utumiaji wao wa huduma za kibenki upo chini.
Naye Katibu wa Chama Kikuu
cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) Bw. Bakari Kadabi aliwaomba
wananchi wote kuungana kutokomeza uvuvi haramu na kuuunga mkono juhudi zinazofanywa
na serikali kuongeza mnyororo wa thamani kwa wavuvi na vikundi kujiunga na
chama kikuu ambapo mkataba huo na TPB utawawezesha wadau wa sekta ya uvuvi
kupata elimu ya fedha na kukopeshwa na benki hiyo kwa ajili ya uendelezaji wa
kazi zao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni