Serikali imewataka maafisa
mifugo wote nchini katika maeneo yao ya kazi kufuatilia idadi ya viwanda vinavyotumia
malighafi ya mifugo ambavyo vinafanya kazi pamoja na ambavyo havifanyi kazi
kufahamu changamoto zake ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi na viwanda hivyo vianze
kufanya kazi kuendana na azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea
viwanda Mwaka 2025.
Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha hayo jana (27.10.2019)
katika Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wakati alipotembelea kiwanda cha
kuchakata mazao ya mifugo cha Rotiana Social Investment ambacho kwa sasa hakifanyi
kazi na baadhi ya mitambo yake kuharibika na vifaa vingine kudaiwa kuibiwa na
baadhi ya watu waliokuwa wakikisimamia kiwanda hicho.
Prof. Gabriel amesema lengo
la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha inasimamia vyema azma ya serikali
kuhakikisha viwanda vya malighafi za mifugo vinafanya kazi na kutaka maafisa
hao wa mifugo kushirikiana na maafisa kutoka Taasisi ya Biashara, Viwanda na
Kilimo (TCCIA) katika kubaini changamoto mbalimbali zinazovikabili viwanda
hivyo.
“Kwa kushirikiana na ofisi
ya mkuu wa Mkoa wa Manyara umuliki wa mitambo lazima uweze kufahamika kisheria
umekaaje na kuhakikisha viwanda ambavyo vimekuwa vikichakata mazao ya mifugo
vinafanya kazi ili mnyororo wa mazao ya mifugo uendelee kufanya kazi na kufikia
uchumi wa kati 2025 kupitia viwanda.” Amesema Prof. Gabriel
Kuhusu kiwanda cha Rotiana
Social Investment chenye eneo la Hekari 12,500 Prof. Gabriel ameutaka uongozi
wa Mkoa wa Manyara kuendelea kufuatilia kwa kina umiliki wa ardhi wa eneo hilo
kisheria kutokana na kiwanda hicho kutekelezwa baada ya kuibuliwa na Taasisi ya
Ilaramatak Lorkornei na Stitching Her Groen Wout ya nchini Uholanzi na
kufunguliwa kiwanda mwaka 2011 ambapo kwa sasa hakifanyi kazi.
Kiwanda hicho ambacho kina
uwezo wa kuchinja ng’ombe zaidi ya 300 kwa siku na pamoja na mifugo mingine
wakiwemo mbuzi katibu mkuu huyo ametaka pia uongozi wa Mkoa wa Manayara
kufuatilia kwa kina umiliki wa mitambo hiyo kisheria na hatimaye kiwanda hicho
kiweze kufanya kazi baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Bibi Mary Kisyoki ambaye
amewahi kuwa mmoja wa viongozi wa Shamba la Rotiana linalomiliki kiwanda cha
Rotiana Social Invetment ameshukuru uongozi wa Mkoa wa Manyara na TCCIA katika
kufuatilia kiwanda hicho kilichotelekezwa ambapo amesema kupitia serikali ya
awamu ya tano ataendelea kusimamia ukweli ambao amekuwa akiusimamia katika
kulinda mali za kiwanda hicho zinasimamiwa vyema na hatimaye kiweze kufanya
kazi.
Amesema katika kipindi
chote mara baada ya kiwanda hicho kusimama kufanya kazi amekuwa akihakikisha
mali za kiwanda hazizidi kuibiwa au kuharibiwa na baadhi ya watu.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Manyara Bibi Mwanahamisi Hussein ametoa wito kwa
makatibu wenzake wa mikoa na wilaya kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali na
sekta binafsi na kujikita kuangalia fursa na changamtoto zilizopo ili kuweza kuzitatua
zikiwemo za wafugaji na kuhakikisha jamii inapata faida kutokana na yale
wanayosimamia.
Aidha ameishuru Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa kuweza kufuatialia masuala mbalimbali kwa kuweza kufanyia
kazi yale ambayo yamekuwa yakifikishwa katika wizara hiyo likiwemo la
kutekelezwa kwa kiwanda cha Rotiana Social Investmant suala ambalo amekuwa
akilisimamia ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafahamika umiliki wake na
hatimaye kiweze kufanya kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni