SERIKALI imeamua
kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009
ili kuondoa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji katika sekta ya uvuvi ili
kwenda na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya awamu ya tano inayolenga kujenga
Tanzania ya viwanda na kuwatetea, kuwalinda wanyonge.
Akizungumza katika
uzinduzi zoezi la ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu rasimu ya Sheria ya Uvuvi na
Sheria ya Ukuzaji viumbe kwenye maji katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es
Salaam jana Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametaja sababu nyingine
zilizosababisha kuwepo mabadiliko hayo.
Ni pamoja na kutoa
ulinzi madhubuti wa rasilimali za uvuvi, kuongeza uzalishaji na kuwa na masoko
ya uhakika sambamba na kudhibiti utoroshwaji na uingizaji holela wa mazao ya
uvuvi nchini.
Aidha Waziri Mpina
alisema sheria hiyo mpya inatakiwa iendane pia na mabadiliko na matumizi ya
sayansi na teknolojia katika uvuvi na ukuzaji viumbe kwenye maji ili kwenda
sambamba na mahitaji pamoja na kuwepo mwamko mkubwa wa ufugaji wa samaki kwenye
maji uliojitokeza miongoni mwa wananchi.
Alisema pamoja na
rasimu ya sheria hizo mbili pia Serikali iko kwenye hatua za mwisho za
kufazifanyia marekebisho Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Namba 29
ya mwaka 1994 na Kanuni zake za mwaka 2009 na Sheria ya Bahari Kuu Cap 388 na
Kanuni zake za mwaka 2007 na 2016.
Hivyo Waziri Mpina
aliwasihi wananchi kutoa maoni yasiyofungamana na upande wowote na kuacha tabia
ya kila mmoja kuvutia upande wake ili kuwezesha kutunga sheria madhubuti.
Aidha Waziri Mpina
alieleza utajiri wa kipekee wa rasilimali za uvuvi hapa nchini ikiwemo kuwa na
eneo kubwa la maji lenye kilomita za mraba 346,337 sawa na asilimia 36.7 ya
eneo lote la nchi yetu, fukwe ndefu na za kuvutia, kuwepo kwa samaki na viumbe
vingine ambavyo vimetoweka na vingine vikiwa kwenye tishio la kutoweka duniani.
Pia kuwepo kwa
mito, mabwawa na maziwa yenye sifa za kipekee ikiwemo Ziwa Victoria ambalo ni
la pili kwa ukubwa duniani na Ziwa Tanganyika ambalo ni la pili kwa kina
duniani na la kwanza kwa ujazo wa maji duniani.
Hivyo alisisitiza
kuwa wakati nchi inakwenda kutunga sheria hiyo mpya ya uvuvi ni muhimu kama
Taifa kujiuliza maswali kadhaa ikiwemo matumizi sahihi ya rasilimali hizo.
“lazima tujiulize
tunapata wapi uhalali wa kuagiza samaki kutoka nje ya nchi?, tujulieze kwa nini
tumeshindwa kulihudumia soko la ndani na la nchi jirani, Afrika na dunia?, kwa
nini tuzidiwe uzalishaji na mauzo na nchi ambazo tunazizidi kwa mbali kwa
rasilimali?”alihoji Mpina,
“Vilevile Kwanini
tuwe na wavuvi masikini tena ambao hawana zana bora za uvuvi, kwanini biashara,
uwekezaji na ujenzi wa viwanda ni wa kusuasua ? haya ndio maswali tunayopaswa
kujiuza kama Taifa”alihoji Mpina.
Hivyo Waziri Mpina
alisema kutokana na ugumu wa maswali hayo ndio maana wizara yake ikaamua ni
bora kuifumua Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka
2009 ili kusaidia kupata majawabu ya namna gani kama taifa litatoka kwenye
mkwamo huo.
Wakichangia rasimu
hiyo iliyowahusisha wavuvi, wachakataji wa samaki, wauza zana za uvuvi,
wafugaji wa samaki kwenye maji, wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, wakuu wa
wilaya, wakurugenzi wa halamshauri, wawakilishi wa vyuo vikuu na viongozi wa
dini.
Wakizungumzia
mapungufu ya sheria hiyo baadhi ya wadau wa wavuvi walisema sheria imekataza
matumizi ya taa za sola, jenereta pamoja na utitiri wa leseni hali iliyochangia
wavuvi wengi kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yao.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa aliipongeza
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kubuni wazo hilo na kusisitiza kuwa wao kama
Bunge wako tayari kushirikiana na Serikali katika kubadilisha sheria zote
zinazokwamisha juhudi za kujenga Tanzania ya viwanda huku akisitiza wadau
kutumia vizuri fursa hiyo na kwamba wasijitoe katika uandaaji wa sheria hizo
mpya.
Katibu Mkuu Uvuvi,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama alisema atasimamia kikamilifu
uratibu wa zoezi zima la ukusanyaji maoni ya wadau na kwamba timu ya wataalamu
wa wizara hiyo itaenda kila mahali walipo wadau.
Aidha Dk Tamatamata alisema zoezi hilo kwa ukanda wa Ziwa
Victoria lilizinduliwa na Waziri Mpina Januari 28 mwaka huu ambapo wadau
walijitokeza kutoa maoni yao na kwamba zoezi hilo litaendelea hadi Februari 28
mwaka huu huku akisisitiza maoni yanakaribishwa kwa maandishi kupitia barua
pepe ya maoni@uvuvi.go.tz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni