WAZIRI wa Mifugo na
Uvuvi, Luhaga Mpina, amezindua Mpango Kambambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo
nchini (Tanzania Livestock Master Plan-TLMP) huku akimtaka Katibu Mkuu Mifugo
kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati huo ndani ya siku 30 ili utekelezaji
uanze mara moja.
Akizindua mpango
huo jijini Dar es Salaam, Waziri Mpina alisema, ni lazima mpango mkakati wa
utekelezaji uwasilishwe ofisini kwake ndani ya kipindi hicho ili kuondoa dhana
iliyojengeka ya mipango mingi kuandaliwa kwa muda mrefu na gharama kubwa,
lakini usimamizi na utekelezaji wake kuwa dhaifu na kushindwa kuleta matokeo
yaliyotarajiwa.
Alisema Tanzania
ina mifugo mingi, ikiwa na asilimia 1.4 ya ng'ombe duniani na asilimia 11 ya
ng'ombe Bara la Afrika wako Tanzania huku ikiwa ya pili barani Afrika baada ya
Ethiopia.
Waziri Mpina
alisema fursa na changamoto zimefanikisha kuandaliwa kwa mpango huo ili kuondoa
vikwazo na kuweka mazingira wezeshi ya ufugaji, biashara na uwekezaji.
Alizitaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa malisho na maji, wafugaji
kufukuzwa kila mahali, ukosefu wa dawa na chanjo za mifugo, ongezeko la bidhaa
za mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi, uwekezaji wa kusuasua, ukosefu wa bei
nzuri, soko la uhakika na mitaji na ukosefu wa mifugo iliyoboreshwa na huduma
za utafiti.
Aliwataka wadau wa
maendeleo waliofadhili mpango huo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo
(ILRI) na Taasisi ya Bill & Melinda Gate Foundation, kutoishia kufadhili
uandaaji wa mpango huo badala yake washiriki moja kwa moja kwenye utekelezaji
wake.
Pia aliwataka
watendaji wote wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa kujipanga na kushiriki katika
utekelezaji wa mpango huo ili kuleta matokeo ya haraka.
Waziri Mpina pia
aliitaka sekta binafsi, wafugaji, jumuiya za wafugaji, wafanyabiashara,
wawekezaji, taasisi za fedha kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kutekeleza
mpango huo.
Kufuatia mpango
huo, serikali italazimika kufanya marekebisho ya sera na sheria pamoja na
kuanzisha mikakati na miongozo mipya ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo
kwa ufanisi mkubwa.
Naye Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema kuzinduliwa kwa
mpango huo kumeiwezesha wizara yake kupanga matumizi bora ya ardhi ili kufanikisha
utekelezaji wa mpango huo.
"Ardhi yangu
haina maana kama haitumiki vizuri, mimi nafurahi sasa mmejipanga na
mmetengeneza mpango mzuri ambao utasaidia hata kunipa kazi ya kupanga matumizi
ya kufanikisha mpango wenu, nataka nikuhakikishie mheshimiwa Mpina tuko pamoja
najua mahitaji yenu,” alisema Lukuvi.
Katibu Mkuu Mifugo,
Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema mpango huo ulianza kuandaliwa miaka mingi
iliyopita, lakini sasa umekamilika na kuzinduliwa huku akimhakikishia Waziri
Mpina kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wake ili kuleta matokeo ya haraka
yanayotakiwa na Watanzania.
Kwa upande wao
mawaziri wastaafu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani na Dk. Charles
Tizeba, walimpongeza Waziri Mpina kwa kufanikisha mpango na kukiri kuwa Wizara
ya Mifugo na Uvuvi sasa imejizatiti kusimamia sheria, hatua itakayoiwesha
kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
Wenyeviti wa CCM,
mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamepongeza mpango huo na kusisitiza kuwa CCM
kinathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na waziri Mpina katika kuleta
mageuzi ya kweli katika sekta ya mifugo nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, George Bajuta
alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa jitihada anazofanya za kuwasaidia
wafugaji nchini huku akimpongeza waziri Mpina kwa kuendelea kuwa kielelezo cha
mageuzi katika sekta ya mifugo nchini.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akizindua Mpango Kambambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini (Tanzania Livestock Master Plan-TLMP) |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni