Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) ni ugonjwa
hatari kwa binadamu na mifugo hususan ng’ombe, mbuzi, kondoo na ngamia ambao
husababishwa na virusi jamii ya Bunyaviridae.
Wanyama huambukizwa kwa kuumwa na mbu aina ya ‘Aedes”. Binadamu hupata ugonjwa
kwa kushika au kula nyama ya mnyama aliyeambukizwa na virusi vya ugonjwa huo
Katika siku za hivi Mamlaka ya Hali ya Hewa Kenya, Shirika
la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wametoa taarifa za matukio ya
ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF)
Kaskazini mwa Kenya na Mashariki mwa nchi ya Rwanda. Hata hivyo Ugonjwa huo haupo hapa nchini.
Kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huu katika nchi jirani,
Wizara inatoa maelekezo yafuatayo kwa Halmashauri zote nchini (Idara
za Mifugo, Afya na Elimu) na mikoa yote kuzingatia yafuatayo ili kuchukua
tahadhari zote zinazotakiwa ili ugonjwa huu usiweze kuingia nchini.
(a) Halmashauri
zianze kutoa taarifa na elimu kwa umma, hasa kwa wadau wote wanaofanya shughuli
za Mifugo, Utoaji wa huduma za Afya n.k. juu ya njia za kudhibiti maambukizi au
mlipuko wa ugonjwa huu.
(b) Halmashauri kuhimiza
Wafugaji kuogesha mifugo yao mara kwa mara kwa kutumia viuatilifu (vyenye kiini
cha pareto/pyrethroids) ili kudhibiti kupe, mbu, mbung’o na visumbufu wengine
waenezao magonjwa.
(c) Kuwaagiza
Wananchi kutoa taarifa haraka kwa Wataalamu wa Mifugo, Vituo vya Huduma za Afya
au Vituo vya Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo mara wanapoona vifo vingi vya
ghafla kwa wanyama, kutupa au kuharibu mimba na wengine kuzubaa kwa homa kali.
(d) Halmashauri kutoa
elimu kwa Umma na kuhahakisha wanyama wote wanachinjiwa machinjioni na wapimwe na
nyama yao pia ipimwe na Mtaalamu wa Mifugo kabla na baada ya kuchinjwa. Aidha, nyama
zinunuliwe kwenye bucha au super-markets zilizoidhinishwa na sio mitaani.
(e) Kamati za
majanga/maafa za Wilaya ziimarishwe na kwa kushirikiana na Wadau wengine
wafuatilie mwenendo na matukio ya magonjwa katika Wilaya zao na kutoa taarifa
kwa Wizara husika
IMETOLEWA NA:
Dkt. Mary S.H. Mashingo
KATIBU MKUU
(MIFUGO)
WIZARA YA
MIFUGO NA UVUVI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni