Na. Stanley Brayton
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega amekabidhi chanjo ya ugonjwa wa kimeta kwa waathirika wa
mafuriko ya Hanang yaliyotokea mwishoni mwa mwaka uliopita mkoani Manyara
zilizokabidhiwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho,
Bw. Gabriel Bura Januari 04, 2023.
Bw. Bura amekabidhi chanjo
hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga ambaye ameishukuru Wizara
kwa kuwapatia msaada wa chanjo hiyo itakayokuwa msaada kwa Mifugo iliyoathiriwa
na maporomoko ya tope yaliyotokea mkoani humo.
"Tumeleta Chanjo ya
Ugonjwa wa Kimeta (Anthrax), Dozi 20,000 kwa ajili ya Mifugo ya wakazi wa
Hanang waliopatwa na janga la maporomoko ya matope kama Mheshimiwa Waziri Ulega
alivyohaidi na kama sote tunavyofahamu kupitia wadau mbalimbali, Wizara
imeshatoa misaada ya ng'ombe, mayai, maziwa na fedha taslimu hivyo kinachofuata
sasa katika kurejesha hali kwa waathirika, ni kuhakikisha ile Mifugo
iliyonusurika inakuwa salama na haitopata madhara" Alisema Bura.
Akizungumza mara baada ya
kupokea chanjo hizo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga ameishukuru
Wizara kwa msaada huo ambapo ametoa maelekezo kwa wahusika kuzielekeza kwenye
maeneo yaliyoathirika.
"Ninaishukuru
sana Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa
sababu hii sio mara ya kwanza mnakuja kutoa misaada hapa Hanang tangu janga
hili litokee hivyo ninaagiza idara husika itafute maeneo ambayo mifugo
imeathirika ili kuzuia ugonjwa huu wa Kimeta usienee" alisema Mhe. Sendiga
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bi. Rose Kamili, ameishukuru Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya wananchi wa Hanang na kuahidi kuzielekeza chanjo
hizo kwenye maeneo yote yaliyoathirika.
"Tunawaahidi
kusimamia, chanjo hizo katika vijiji vyetu vyote, ambavyo vinahitaji uchanjaji
wa Mifugo ili kuweza kuzuia magonjwa kuliko kusubiri kutibu" Alisema Bi.
Rose
Naye Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bw. Francis Namaumbo amesema kuwa mbali na
chanjo hizo kuisaidia mifugo iliyoathiriwa na mafuriko zitawasaidia kulinda
afya ya walaji ambao wangeathirika kutokana na matumizi ya nyama inayotokana na
mifugo yenye ugonjwa huo.
Na vilevile, anaishukuru
Wizara kwa kuleta pikipiki 10, kwa ajili ya maafisa ugani ili kuweza kutoa
huduma.
Naye mkazi wa Kata ya
Ganana, ambae pia ni mfugaji, Bw. Fabiano Sule mbali na kuishukuru Serikali kwa
msaada huo, ameiomba kuendelea kuwapatia chanjo za magonjwa ya ngozi kwa
ng'ombe yaliyotokana na mifugo hiyo kunywa maji au kula udongo karibu na maeneo
yalioathiriwa.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Mhe. Queen Sendiga (katikati), akipokea msaada wa chanjo ya ugonjwa wa kimeta
(Anthrax) kwa ajili ya kuchanja Mifugo, kutoka kwa mwakilishi wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji wa Maeneo ya
Malisho, Bw. Gabriel Bura, misaada hiyo imekabidhiwa katika Ofisi za
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara, Januari 04, 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Mhe. Queen Sendiga (katikati), akishukuru baada ya kupokea msaada wa chanjo ya
ugonjwa wa kimeta (Anthrax) kwa ajili ya kuchanja Mifugo, kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Januari 04, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni