Nav bar

Jumamosi, 2 Septemba 2023

ELIMU KUHUSU PROGRAMU YA UTOAJI CHANJO DHIDI YA MAGONJWA YA WANYAMA YA KIPAUMBELE YAANZA KUTOLEWA

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutoa elimu kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele ambayo inatarajiwa kuanza kwa lengo la kudhibiti magonjwa ya mifugo.

 

Hayo yamesemwa leo (01.09.2023) na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina baada ya kumalizika kwa semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

 

Dkt. Mhina amesema malengo makubwa ya Wizara ni kuhakikisha mifugo haipotezi ubora au kufa kutokana na magonjwa wakati hayo yote yanaweza kuzuilika kupitia utoaji wa chanjo. Hivyo kupitia program hii ya uchanjaji tatizo la magonjwa kwa mifugo litakuwa limedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

 

“Katika semina hii tuliyoifanya kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo tumeweza kupokea maoni mengi yatakayosaidia utekelezaji wa program hii, kama namna ya upunguzaji wa gharama za chanjo na suala zima la utoaji wa elimu ya umuhimu wa uchanjaji mifugo kwa wafugaji na wadau wote wa sekta ya mifugo ili wote kwa ujumla wazingatie kalenda ya chanjo,” alisema

 

Dkt. Mhina amewahimiza wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao ili wawe na mifugo iliyokidhi vigezo vya kiafya vya kitaifa na kimataifa ambapo pia magonjwa kutoka kwenye mifugo kwenda kwa binadamu yatakuwa yamezuiliwa. Vilevile chanjo hizi zitasaidia kuongeza ubora wa mifugo na mazao yake na hivyo kukidhi viwango na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Kuongezeka kwa ubora wa mifugo na mazao yake kutasaidia kuongeza kipato kwa wafugaji na mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariamu Ditopile Mzuzuri ameipongeza Wizara kwa kuandaa semina kuhusu Programu ya Utoaji Chanjo dhidi ya Magonjwa ya Wanyama ya Kipaumbele kwa wajumbe wa kamati hiyo kwani imesaidia kuwaongezeaa uelewa kuhusu shughuli zinazofanywa na sekta ya mifugo.

 

Bi. Mzuzuri amesema suala la chanjo ni muhimu sana kuzingatiwa na wafugaji, hivyo ni lazima kwanza elimu ya kutosha itolewa kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo na madhara ya kutochanja mifugo kwa kuzingatia kalenda iliyowekwa. Pia amesema kuwa zipo fursa nyingi katika mnyororo mzima wa biashara ya mifugo na mazao yake ambayo ikitumiwa vizuri itasaidia hata katika kutatua tatizo la upungufu dola lililopo hapa nchini na pia kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.

 

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Hester inayozalisha chanjo za mifugo, Bi. Tina Sokoine amesema kuwa wamekuwa na majadiliano mazuri na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ambapo wameweza kuelezea shughuli za uzalishaji wa chanjo zinazotengenezwa na Kampuni hiyo. Sokoine amesema kiwanda hicho kinazalisha chanjo 26 ikiwa ni pamoja na chanjo za magonjwa zaidi ya saba ya kipaumbele hapa nchini ambazo zote huuzwa ndani na nje ya nchi.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (kushoto) akitoa salam za Wizara kwenye semina kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma. Dkt. Mhina amesema Wizara imedhamiria kusimamia program ya chanjo ili kuwa na mifugo na mazao ya mifugo yaliyo bora kwa mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga. (01.09.2023)


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariamu Mzuzuri akifunga semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele ambapo amesisitiza suala la utoaji elimu kwa wafugaji ili watambue umuhimu wa chanjo kwa mifugo na kuhakikisha wanafuata kalenda ya chanjo. (01.09.2023)


Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga (wa pili kulia) akiwasilisha mada kwenye semina kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma. Prof. Nonga ameelezea namna Wizara ilivyojipanga kuendesha program hiyo yenye lengo la kudhibiti magonjwa ya mifugo hapa nchini. Wa kwanza kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina. (01.09.2023)


Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Chanjo – HESTER, Bi. Tina Sokoine (wa pili kushoto) akiwasilisha mada kuhusu hali ya uzalishaji wa chanjo za mifugo katika kiwanda hicho wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele iliyotolewa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Bungeni Jijini Dodoma. (01.09.2023)


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele. Semina hiyo imefanyika Bungeni Jijini Dodoma. (01.09.2023)


Picha ya pamoja ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariamu Mzuzuri (wa nne kutoka kulia), Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina (wa pili kutoka kushoto), Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Wataalam wa Wizara na Kampuni ya HESTER mara baada ya kumalizika kwa semina kuhusu program ya utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya wanyama ya kipaumbele iliyofanyika Bungeni Jijini Dodoma. (01.09.2023)
#MifugoNaUvuviNiUtajiri

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni