Nav bar

Jumapili, 27 Agosti 2023

SERIKALI YAANZA MAANDALIZI YA MAPITIO YA SHERIA NA SERA YA UVUVI

◼️ Ni hatua ya kuelekea uanzishwaji wa mamlaka ya Uvuvi nchini 


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza maandalizi ya mapitio ya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 na Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 ili kuziboresha na kuzifanya na mwelekeo mmoja.


Maandalizi hayo yameanza kufanyika kuanzia leo Agosti 10-11, 2023 mkoani Morogoro kwenye warsha inayojumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya Uvuvi chini ya uratibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO).


Akizungumza wakati wa kufungua Warsha hiyo Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga amesema kuwa maboresho hayo yanalenga kuifanya sekta ya Uvuvi kuendana na mabadiliko ya Sayansi na teknolojia yanayoendelea kujitokeza kila uchwao.


"Kutokana na sababu hiyo tumejikuta sekta yetu imekuwa nyuma kwenye mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na jambo hili hatuwezi kulifanya sisi kama Wizara peke yetu ndo maana tumeshirikisha Vikundi vya ulinzi wa rasilimali za Uvuvi, wenzetu wa sekta binafsi na mashirika yasiyo ya Serikali ambayo tumekuwa tukishirikiana nayo" Amesema Lukanga.


Aidha Lukanga amebainisha kuwa maboresho hayo ya Sera na Sheria ya Uvuvi ni sehemu ya maandalizi ya mpango wa Wizara wa kuanzisha mamlaka ya Uvuvi ambapo amewataka wadau wote wazingatie hilo wakati wa mchakato wa kupitia Sera na sheria hiyo.


"Ukiangalia kwenye sera yetu ya mwaka 2015 imetaja mamlaka lakini ukiangalia sheria imetaja Jeshi Usu hivyo tunaona zimetofautiana wakati wenzetu wa maliasili wana mamlaka na Jeshi Usu kwa hiyo na sisi ni lazima Sera na Sheria yetu ivitaje hivyo vyote kwa sababu mpaka sasa imekuwa ni kama rasilimali ambayo haina mwenyewe tofauti na Uvuvi kwa upande wa ukuzaji viumbe maji" Ameongeza Lukanga.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo ulimwenguni (FAO) Dkt. Oliver Mkumbo amesema kuwa suala la uratibu wa Uvuvi endelevu nchini ni zaidi ya Sera na Sheria kwa sababu linahitaji kujitoa kwa wadau wote kuanzia Serikalini, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.


"Hivyo kwa pamoja tunaweza kusimamia vema Sera na Sheria ambazo tumeanza mchakato wa kuzipitia huku tukiendelea kuzingatia na kufanyia kazi mahitaji na changamoto zinazoikabili sekta ya Uvuvi hapa Tanzania bara" Ameongeza Dkt. Mkumbo.


Kufanyika kwa Warsha hiyo ya mapitio ya Sera na Sheria ya Uvuvi nchini ni miongoni mwa hatua ambazo Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kuzichukua ili kuhakikisha rasilimali zinazotokana na uvuvi wa asili zinalindwa.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa warsha ya maandalizi ya mapitio ya Sera na Sheria ya Uvuvi nchini inayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Agosti 10-11, 2023. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO) Dkt. Oliver Mkumbo na kushoto kwake ni Mteknolojia Mkuu wa Samaki nchini Bi. Florah Luhanga.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali muda mfupi baada ya kufungua Warsha ya maandalizi ya mapitio ya Sera na Sheria ya Uvuvi nchini inayofanyika mkoani Morogoro kuanzia Agosti 10-11, 2023. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO) Dkt. Oliver  Mkumbo na kushoto kwake ni Mteknolojia Mkuu wa Samaki nchini Bi. Florah Luhanga.

Sehemu ya Washiriki wa Warsha ya maandalizi ya mapitio ya Sera na Sheria ya Uvuvi nchini  wakifuatilia moja ya taarifa zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye warsha hiyo leo Agosti 10, 2023 mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni