Nav bar

Alhamisi, 24 Agosti 2023

BBT- LIFE ITAFANYA MAPINDUZI YA UFUGAJI-SILINDE

◼️Agusia Nanenane mwakani kuwa ya kimataifa 


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amebainisha kuwa programu ya kujenga kesho iliyo njema kwa wajasiriamali wanawake na vijana kupitia sekta za Mifugo na Uvuvi maarufu kama BBT-LIFE itakuwa chachu ya mabadiliko kwa wafugaji kuachana na mtindo wa kuchunga na kuingia kwenye mfumo wa ufugaji wa kisasa.


Mhe. Silinde amebainisha hayo Agosti 02, 2023 mkoani Morogoro alipotembelea Maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (NaneNane) kanda ya Mashariki ambapo amesema kuwa vijana watakaohitimu kwenye kila awamu kupitia programu hiyo watakuwa mabalozi wazuri watakaporejea kwenye maeneo yao.


"Watu wengi huamini baada ya kuona na ndio maana na sisi tunaamini kupitia mafunzo ya ufugaji wa kisasa wanayopatiwa vijana hawa, wafugaji wengi wanaoendelea na ufugaji wa kuchunga wataenda kubadilika hasa baada ya kuona tija inayopatikana kupitia ufugaji wa kisasa" Amesisitiza Mhe. Silinde.


Wakati huo huo Mhe. Silinde amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi inakusudia kushirikisha nchi jirani kwenye Maonesho ya kitaifa ya Wakulima, wafugaji na wavuvi (NaneNane) kuanzia Mwakani.


"Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa fursa wadau wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi waliopo kwenye nchi hizo kuja kuonesha namna wanavyotekeleza shughuli hizo kwenye nchi zao na kutoa fursa kwa watu wetu kupata bidhaa mbalimbali kutoka huko" Amesema Mhe. Silinde.


Ameongeza kuwa hatua hiyo pia itawapa fursa wakulima, wafugaji na wavuvi waliopo nchini kupata jukwaa la kuuza bidhaa zao kwa wadau wa sekta hizo kutoka nchi jirani.


Maonesho ya kitaifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu isemayo "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo endelevu ya Chakula".

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge (kushoto) wakielekea kuangalia mabanda mbalimbali yaliyopo kwenye Viwanja vya Nanenane mkoani Morogoro yanakofanyika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa upande wa Kanda ya Mashariki Agosti 02, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akiangalia moja ya vinywaji vinavyotengenezwa na zao la Mwani muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye Viwanja vya NaneNane mkoani Morogoro yanakofanyika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa upande wa Kanda ya Mashariki Agosti 02, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akiangalia moja ya viatu vinavyotengenezwa na kiwanda cha "Kilimanjaro Leather" muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Jeshi la Magereza lililopo kwenye Viwanja vya NaneNane mkoani Morogoro yanakofanyika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa upande wa Kanda ya Mashariki Agosti 02, 2023.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) akinywa maziwa yanayotengenezwa na Jeshi la Magereza muda mfupi baada ya kufika kwenye banda hilo lililopo kwenye Viwanja vya NaneNane mkoani Morogoro yanakofanyika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa upande wa Kanda ya Mashariki Agosti 02, 2023.

Mtengenezaji wa mifumo ya kufuga samaki katika maeneo madogo Bw. Gasana Damian (kushoto) akimueleza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (katikati) namna mifumo hiyo inavyofanya kazi wakati wa ziara ya Mhe.Silinde kwenye Viwanja vya NaneNane mkoani Morogoro yanakofanyika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa upande wa Kanda ya Mashariki Agosti 02, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni