Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imetakiwa kuwasimamia vizuri vijana 240 wanaoendelea kupatiwa mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika vituo atamizi 8 chini ya LITA ikiwa ni mpango wa Serikali kusaidia vijana hao kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa LITA kilichofanyika mkoani Arusha Mei 26, 2023.
Dkt. Mhina alisema Serikali imeanza kutekeleza mradi huo katika mwaka huu wa fedha baada ya kubaini wataalamu wanaotoka katika vyuo hivyo wanayo nafasi ya kupatiwa ujuzi zaidi ya kuzalisha kupitia vituo atamizi ili watakaporejea mitaani waweze kuwa na uwezo wa kuwekeza zaidi.
“Tunatengeneza wataalam ambao ni wawekezaji wao wenyewe watakapoweza kuzalisha ndivyo ambavyo tutaweza kuzalisha malighafi zaidi kwenye viwanda vyetu, kwahiyo hatutarajii wakitoka hapa wakategemee kuajiriwa ndio maana tunawaweka kwenye vituo atamizi ili wafanye kwa vitendo na kufanya kibiashara zaidi” amesema
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene alifafanua kuwa mradi huo kwa kuanzia utatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo utagawanywa kwa awamu 4 ambapo vijana hao watahudumia mifugo kwa kunenepesha ndani ya miezi 3.
Alisema katika kila kituo kuna vijana wasiopungua 30 ambapo kila mmoja anahudumia ng’ombe 10 kwa kuwanenepesha kwa kipindi cha miezi mitatu na kufanya wahudumia ngombe 40 kwa mwaka mzima
“ kila kijana kwa mzunguko moja amepewa ng’ombe 10 wa kunenepesha kwa hiyo kwa mwaka mzima atanenepesha ngombe 40 na tunategemea faida itakayotokana na hao Ng’ombe watakao uzwa mnadani ni mtaji kwa kijana kwa ajili ya kwenda kuanzisha mradi wake baada ya kumaliza mwaka mmoja” amesema
Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa fursa nzuri kwa vijana kufuga kibiashara kwa sababu licha ya kuanza kutekeleza mradi huo mwezi Aprili mwaka huu tayari wameanza kupokea oda ya kuhitaji ng’ombe hao.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA),
Dkt. Pius Mwambene (kulia) akieleza namna wakala hiyo inavyotekeleza majukumu
yake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa vitendo ili kuwaandaa vijana kujiajiri,
kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina wakati
alipoenda kufungua kikao cha baraza la wafanyakazi LITA kilichofanyika Tengeru
mkoani Arusha Mei 26,2023.
Mwanafunzi anayejikita kwenye eneo la Afya ya Mnyama na
Uzalishaji Bw. Julius Mmbando akionyesha namna taarifa /majibu ya vipimo vya
magonjwa mbalimbali ya mnyama yanavyotoka kwenye mashine ya kupimia magonjwa
hayo ya mifugo kwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu Dkt. Charles Mhina alifika chuoni
hapo Tengeru Mkoani Arusha Mei 26,2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni