Nav bar

Alhamisi, 6 Aprili 2023

ZIARA YA DKT. SAMIA NCHINI QATAR YAVUTA WAWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona


Ziara ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya Mwezi Oktoba, 2022 nchini Qatar imeendelea kuvuta wawekezaji kutaka kuja kuwekeza kwenye sekta ya mifugo hapa nchini.


Hilo limefahamika baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Widam Food, Bw. Al Noubay Al Marri kutoka nchini Qatar  kumtembelea Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega jijini Dodoma Aprili 4, 2023.


Akiongea katika kikao baina yake na Waziri Ulega alisema kuwa uamuzi wake wa kutaka kuwekeza hapa nchini ulipata msukumo kufuatia ziara ya   Mhe. Rais, Dkt. Samia aliyoifanya nchini Qatar.


Alisema lengo la ziara yake  ni kukamilisha hatua za kuanzisha kampuni ya Widam Food hapa nchini ambayo inashughulika na biashara ya Nyama.


"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutufungulia milango ya uwekezaji hapa Tanzania, na sisi tunaona  Nyama ya Tanzania ina mustakabali mzuri kibiashara nchini Qatar," alisema Al Noubay


Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alisema Serikali ya Rais Samia imedhamiria kuboresha uzalishaji wa sekta ya Mifugo hivyo ujio wa Mkurugenzi huyo unaunga mkono jitihada za serikali.


"Sisi tunawakaribisha hapa Tanzania, Rais Samia ameshafungua njia, kilichobaki ni sisi kuwawezesha nyinyi ili uwekezaji wenu uweze kufanikiwa," alisema Mhe. Ulega


Aidha, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo pia kumuahidi ushirikiano Mkurugenzi huyo huku akimueleza kuwa akihisi kupata changamoto yoyote asisite kuijulisha wizara ili waweze  kuitatua.


Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati kulia) akiongea na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Widam Food, Bw. Al Noubay Al Marri kutoka nchini Qatar alipokutana nae ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 4, 2023. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Widam Food, Bw. Al Noubay Al Marri (kushoto) kutoka nchini Qatar walipotembelea Machinjio ya Dodoma yaliyopo  jijini Dodoma Aprili 4, 2023

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Widam Food, Bw. Al Noubay Al Marri kutoka nchini Qatar akimueleza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) lengo la ziara yake  alipotembelea ofisini kwake jijini Dodoma Aprili 4, 2023.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni