Nav bar

Alhamisi, 13 Aprili 2023

WAFUGAJI WATAKIWA KUJUA NYAMA NI DILI, WAFUGE KIBIASHARA

Wafugaji wametakiwa kujua kuwa soko la nyama inayozalishwa hapa nchini limefunguka hivyo wajipange kubadilika na kufanya ufugaji wa kibiashara ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji.


Rai hiyo ilitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega wakati wa hafla ya kugawa madume kwa vikundi vya wafugaji iliyofanyika  katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mkoani Singida Aprili 6, 2023.


"Ndio maana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Tshs. Milioni 878. 4 kwa ajili ya  kununua haya madume bora 366 ili wafugaji tuweze kuboresha mifugo yetu, tuweze kupata ng'ombe wanaoweza kutoa nyama nyingi na kufanya biashara yenye tija kuliko hivi sasa", alisema


Aliongeza kwa kusema kuwa madume hayo yatawawezesha wafugaji kuwa na ng'ombe chotara ambao wanauwezo wa kuzalisha wastani wa kilo 150- 200 za nyama ukilinganisha na uzalishaji wa kilo 80-120 kwa Ng'ombe wa asili. 


"Mifugo ni uchumi, na leo nawaambieni nyama ni dili, Rais Samia amefungua milango, wakati huu tunapokea wageni wengi kutoka nje ya nchi wakitaka kufanya biashara ya nyama na nchi yetu", alifafanua Ulega


Naye, Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga alimshukuru Waziri Ulega kwa kuwezesha wafugaji wa Wilaya ya Mkalama kupata madume Bora 40 huku akimuahidi kuwa watayatumia vizuri madume hayo kuboresha uzalishaji wa mifugo yao.


Halmashauri nyingine zilizopata  mgao huo ni pamoja na Mkuranga 50, Mvomero 40, Buchosa 46, Chamwino 50, Maswali 50, Chato 50 na Msalala 50.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni