Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewahakikishia wananchi wa Kijiji cha Mekomariro kuwa eneo la Kituo cha Kupumzishia Mifugo Buhemba kuwa halijauzwa na hakuna muwekezaji yeyote aliyepatiwa eneo hilo.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (07.01.2023) wakati alipokuwa
kwenye ziara ya kikazi kwenye Wilaya Bunda mkoani Mara ambapo alizungumza na
wananchi wa Kijiji cha Mekomariro waliokuwa wakilalamika kuwa eneo hilo limechukuliwa
na mwekezaji.
Waziri Ndaki amewaeleza wananchi hao kuwa eneo hilo
halijauzwa na halijatolewa kwa mwekezaji yoyote. Serikali bado inayo mipango ya
kulitumia eneo hilo kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutengwa kwake. Hivyo
wananchi wametakiwa kuwa watulivu na kutosikiliza maneno yanayozushwa kuhusu matumizi
ya eneo hilo kwa kuwa kama serikali itataka kubadilisha matumizi itatangaza.
Kamati ya Mawaziri Nane (8) wa kisekta iliamua kuwa sehemu ya
eneo hilo la kituo ligawanywe kwa wananchi kwa kufuata taratibu, na eneo linalobakia
liendelee kumilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo).
“Kwa kuwa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ilishatoa maelekezo
ya kuligawanya eneo, Kijiji cha Mekomariro kimepewa hekta 794.92 na Vijiji vya
Mirwa na Magunga vimepatiwa hekta 194.94, hivyo wataalam wanafanya upimaji katika
eneo hilo lengo ni kutambua mipaka ya eneo litakalotolewa kwa vijiji hivyo na
sio kuwatishia wananchi au kumpatia mwekezaji,” alisema
Waziri Ndaki amewataka wananchi hao kuwa watulivu wakisubiri
upimaji unaofanywa kukamilika ili waweze kutambua eneo ambalo wanapatiwa na
kuacha kuvamia eneo hilo na kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi na
kilimo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Joshua Nasari amewataka
wananchi hao kutozalisha migogoro ya ardhi kutokana na kutoheshimu mipango
inayowekwa ya matumizi ya ardhi katika Kijiji.
Nasari amesema kuwa lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya
malisho ya mifugo lakini baadhi ya wanakijiji wanalitumia kwa kujenga makazi na
kilimo, hivyo amewataka wote wanao litumia eneo hilo nje ya utaratibu uliowekwa
kuacha mara moja na kuondoka kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara, ambapo amewaeleza wananchi hao kuwa eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba halijauzwa na hakuna mwekezaji yoyote aliyepatiwa eneo hilo. (07.01.2023)
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Joshua Nasari akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara ambapo amewataka kufuata mipango ya matumizi ya ardhi inayowekwa kwenye vijiji ili migogoro isiwepo. (07.01.2023)
Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Mhe. Boniphace Getere akiwasilisha malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Mekomariro ambapo amesema kuwa wananchi hao wanalalamika kuwa eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba amepewa mwekezaji. (07.01.2023)
Afisa Mifugo Mkoa wa Mara, Yusuph Kuwaya (wa pili kulia) akimuonyesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi eneo la kituo cha kupumzishia mifugo Buhemba wakati alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo. (07.01.2023)
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mekomariro wilayani Bunda mkoani Mara wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji hicho na kuzungumza na wananchi hao. (07.01.2023)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni