◼️ Akiri kuondolewa somo la kilimo elimu ya msingi lilikuwa ni kosa
Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere Bw. Joseph Butiku amekoshwa na hatua ya Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kuanzisha vituo atamizi vitakavyojishughulisha na mafunzo kwa vitendo
kuhusu teknolojia ya unenepeshaji wa Mifugo.
Butiku ameyasema hayo jana
(09.12.2022) ambapo alitumia siku hiyo
ya kumbukizi ya Uhuru wa Tanganyika kutembelea moja ya vituo hivyo
vilivyopo jijini Tanga kwenye Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na
Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Buhuri.
“Sisi wazee wenu tulifanya
makosa makubwa huko nyuma kwa kuwapa elimu ambayo inawahamisha kwenye shughuli
za msingi ambazo ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu jambo ambalo linakinzana na
falsafa ya Mwalimu Nyerere ambayo ilikuwa inasisitiza vijana kuwezeshwa elimu
ya kujitegemea” Amesema Butiku.
Butiku ameongeza kuwa hatua
hiyo ya uanzishwaji wa vituo atamizi ni msingi mzuri wa kukuza uchumi wa
mwananchi mmoja mmoja ambapo mbali na kuwezeshwa maarifa ya ufugaji wa kisasa,
mifugo yao itaongeza malighafi viwandani jambo ambalo litakuza uchumi wa nchi
kwa ujumla.
“Hatutaki vijana ambao
watakuwa wamesoma mpaka ngazi ya shahada ya uzamivu ya mifugo afu bado waingie
mtaani kutafuta ajira wakati huko wanakotoka kwenye maeneo yao hawana hata
shamba la mifugo, hiyo itakuwa ni elimu bandia” Amebainisha Butiku.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt.
Angelo Mwilawa amesema kuwa vituo hivyo vilivyopo jijini Tanga vina jumla ya
vijana 90 ambapo vijana 30 wapo kwenye kituo cha TALIRI na wengine 60 wapo
kwenye kituo cha LITA-kampasi ya Buhuri na lengo la Wizara ni kuhakikisha
vijana hao wanakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za ufugaji kwa kufuata
mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya mifugo.
“Tumeamua kuwashirikisha
vijana hawa kuanzia kwenye hatua ya awali ya ujenzi wa miundombinu yote
watakayoitumia kufuga kabla hatujawapa hiyo mifugo ili iwe rahisi kwao kufanya
hivyo baada ya kutoka hapa kwa sababu tunahitaji wakawe walimu wazuri kwenye
jamii zinazowazunguka huko watakapoenda” Amesema Dkt. Mwilawa.
Taasisi ya Mwalimu Nyerere
ilifanya ziara hiyo kufuatia maelekezo waliyopewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha shughuli za
kiuchumi kwa vijana ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Utafiti,
Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa
(kulia) akimueleza Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bw. Joseph Butiku
kuhusu moja ya malisho ya Mifugo yaliyopo kwenye shamba la Taasisi ya Utafiti
wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Tanga muda mfupi baada ya Bw. Butiku na
ujumbe wake kufika hapo (09.12.2022)
kwa ajili ya kuona maendeleo ya kituo atamizi kilichopo kituoni hapo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere Bw. Joseph Butiku (kulia) akimpa maelekezo Mtafiti Mkuu kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Tanga Bw. Walter
Mangesho muda mfupi baada ya Bw. Butiku na ujumbe wake kufika (09.12.2022) kwa
ajili ya kuona maendeleo ya kituo atamizi kilichopo kituoni hapo.
Mkurugenzi wa Utafiti,
Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa
(kulia) akimueleza Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bw. Joseph Butiku
kuhusu mikakati inayotekelezwa na Wizara kwa ajili ya kuhakikisha uwepo wa
malisho ya mifugo muda mfupi baada ya Bw. Butiku na ujumbe wake kufika kwenye Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini
(TALIRI) kituo cha Tanga kwa ajili ya
kuona maendeleo ya kituo atamizi kilichopo kituoni (09.12.2022).
Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere Bw. Joseph Butiku (mwenye kifimbo katikati) akiwa kwenye picha
ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini
(TALIRI) kituo cha Tanga na vijana waliopo kwenye kituo atamizi kilichopo hapo
muda mfupi baada ya Bw. Butiku na ujumbe wake kuhitimisha ziara yao (09.12.2022)
ambapo walifika kwa ajili ya kuona
maendeleo ya kituo hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni