Nav bar

Jumatano, 21 Desemba 2022

MAAFISA UGANI WATAKIWA KUJITATHMINI KWA KUWAFIKIA WAFUGAJI NA KUONDOA MIGOGORO YA ARDHI

Na. Edward Kondela

Maafisa Ugani wametakiwa kujitathmini na kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata weledi na kushirikiana na wafugaji ili wafugaji hao wafuge kibiashara pamoja na kutokomeza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.


Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi (ACP) Advera Bulimba, amebainisha hayo leo (15.12.2022) wakati akifungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa hao kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma na wengine kutoka sekta binafsi, ambapo amesema baadhi ya kata katika wilaya hiyo zimekuwa zikihusishwa na migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima hivyo kurudisha nyuma jitihada za sekta hizo mbili kukua zaidi.


Kamishna Msaidizi Bulimba ameongeza kuwa ni wakati kwa maafisa ugani kubadilisha fikra zaidi za wafugaji kufuga kisasa na mchango wa Sekta ya Mifugo kuonekana zaidi katika pato la taifa na kubainisha kutoridhishwa na baadhi ya maafisa ugani ambao wanashindwa kufanya jitihada mbalimbali za kutokomeza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi amesema mafunzo rejea kwa maafisa ugani yamekamilika katika Kanda ya Kusini na kwamba wizara inaendelea kutoa mafunzo katika kanda nyingine nchini ili kuhakikisha mafunzo hayo yanawajengea uwezo zaidi maafisa hao kufanya kazi kwa weledi zaidi.


Ameongeza kuwa mapitio ya vigezo vya kupima utendaji kazi wa maafisa ugani ni muhimu katika kupata kipimo sahihi cha utendaji kazi wao kwa kuwa una matokeo ya moja kwa moja kwa wafugaji ambao wanategemea zaidi huduma kutoka kwa maafisa hao ili kubadili fikra katika ufugaji wao.


Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Afisa Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora, Bw. Magesa Makaranga amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao ili kwenda kubadilisha fikra za wafugaji kufuga kwa tija.


Ameongeza kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Mifugo ukiwemo uhaba wa maafisa ugani, watahakikisha wanafanya jitihada za kuwafikia wafugaji popote walipo kadri inavyowezekana na kutatua changamoto za migogoro.


Mkuu wa Wilaya ya Nzenga Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi (ACP) Advera Bulimba akizungumza wakati akifungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) yanayofanyika katika wilaya hiyo yakihusisha maafisa hao kutoka ngazi ya kata kwa Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma, ambapo amewataka kujitathmini na kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata weledi na kushirikiana na wafugaji ili wafugaji hao wafuge kibiashara pamoja na kutokomeza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima. (15.12.2022)


Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi akiwafahamisha baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) wanaoshiriki mafunzo rejea ya siku mbili kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, juu ya umuhimu wa mapitio ya vigezo vya kupima utendaji kazi wa maafisa ugani katika kupata kipimo sahihi cha utendaji kazi wao ambao unakuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa wafugaji. (15.12.2022)


Afisa Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora, Bw. Magesa Makaranga akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake kwenye mafunzo rejea ya siku mbili kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, ambapo amebainisha kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao ili kwenda kubadilisha fikra za wafugaji kufuga kwa tija licha ya uhaba wa maafisa ugani kote nchini. (15.12.2022)


Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bi. Danietta Tindamanyire akizungumzia juu ya mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo na maboresho ya Sera ya Mifugo wakati wa mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani (hawapo pichani) kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, ambapo ametaja mikakati kadhaa ikiwemo ya kuundwa kwa vyama vya ushirika, kuanzishwa kwa mashamba darasa ya mifugo na malisho na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ugani. (15.12.2022)


Picha ya pamoja ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi (ACP) Advera Bulimba, baada ya kufungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa ugani kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma pamoja na washiriki kutoka sekta binafsi na watoa mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi inayoratibu mafunzo hayo. (15.12.2022)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni