Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

WAZIRI MKUU ATOA MAELEKEZO 7 KUIMARISHA ULINZI RASILIMALI ZA UVUVI NCHINI

Na Mbaraka Kambona, Mwanza


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Viongozi na Watendaji wa Mikoa kuhakikisha wanashirikiana kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi na kutokomeza uvuvi haramu ili sekta ya uvuvi iendelee kutoa mchongo mkubwa katika pato la Taifa.


Hayo yalibainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Mkuu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Waziri Mkuu na Watendaji wa Serikali na Wadau wa Uvuvi wa Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.


Kupitia mkutano alitoa maelekezo kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta binafsi kwa maana ya Wavuvi, Wenye Viwanda, Wafanyabiashara ya Samaki, Mazao ya Samaki na zana mbalimbali za uvuvi kama ifuatavyo;


Moja, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ihakikishe inaandaa mikutano ya mara kwa mara itakayokutanisha wadau wote muhimu wa uvuvi kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu changamoto mbalimbali za sekta ya uvuvi na kuzitatua hususan suala la uvuvi haramu.


Mbili, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji kote nchini kuhakikisha kuwa vitendo vya uvuvi haramu vinakomeshwa katika maeneo yao na wote watakaopatikana na makosa ya uvuvi haramu wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sharia.


Tatu, alisema kwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya mapato vya OR-TAMISEMI ni shughuli za uvuvi, kila Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama kuhakikisha hakuna vitendo vyovyote vya uvuvi na biashara haramu kwenye eneo lake.


Nne, Waziri Mkuu aliagiza kila Mkurugenzi wa Halmashauri ahakikishe anatenga na kurudisha asilimia 5 ya mapato yanayotokana na sekta ya uvuvi ili kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi kulingana na miongozo iliyopo.


Tano, Watendaji wote wa serikali watakaothibitika kupokea rushwa kutokana na vitendo vya uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi wa aina yoyote ile watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.


Sita, alitoa wito kwa wavuvi na wadau wa uvuvi kote nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za uvuvi pamoja na sheria nyingine za nchi huku akionya kuwa atakayekamatwa anafanya vitendo vya uvuvi haramu atachukuliwa hatua za kisheria hapo kwa hapo kwa kuwa serikali haitavumilia tena vitendo hivyo.


Saba, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI waendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu ulinzi na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi.


Aidha Waziri Mkuu aliongeza kuwa, kuanzia sasa, pamoja na majukumu mengine, suala la usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi litatumika kupima utendaji wa kazi wa viongozi hao huku akiwataka kuhakikisha kwenye utoaji wa taarifa za utekelezaji wa majukumu yenu suala la usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi katika taarifa za mwezi, robo mwaka na mwaka linajumuishwa na kujidhihirisha ipasavyo.


Mkutano huo wa siku mbili kuanzia Novemba 17-18, 2022 umelenga kujadiliana na kuweka mipango ya kusimamia, kulinda na kuendeleza sekta ya uvuvi ili iendelee kutoa mchango wake katika utoaji wa ajira, chakula na lishe, kipato na pato la Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(Mb) akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima akitoa neno la utangulizi katika Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(Mb) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kutoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah akitoa wasilisho kuhusu Hali ya Sekta ya Uvuvi Nchini kwenye  Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Sehemu ya Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) wakiwa  katika Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Pichani ni sehemu ya wadau walioshiriki katika Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Mkurugenzi wa Uvuvi, Bw. Emmanuel Bulayi akiwaonesha  wadau taa za solar na betri ambazo wavuvi wanazitumia kuvulia dagaa kinyume cha Sheria. Tukio hilo lilifanyika  katika Mkutano wa Waziri Mkuu na Viongozi wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Viktoria uliofanyika Mkoani Mwanza Novemba 17, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni