Nav bar

Ijumaa, 25 Novemba 2022

MAAFISA UGANI KUANZA KUPIMWA KIELEKTRONIKI

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amebainisha kuwa Sekta hiyo inatarajia kuanza kupima utendaji wa Maafisa Ugani wake kwa kutumia mfumo wa kielektroniki hatua ambayo itaongeza ufanisi wa huduma kwa wafugaji.


Nzunda ameyasema hayo leo (17.11.2022) wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa Ugani kutoka Mikoa ya Nyanda za juu kusini tukio lililofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.


“Asilimia kubwa ya Maafisa Ugani mnalipwa mshahara kwa kufanya kazi kidogo sana na kazi zenyewe matokeo yake ni kidogo pia na ndio maana tunataka kuimarisha mfumo wa huduma za ugani na kwa kuanzia tutasajili Maafisa ugani na wafugaji wote kwa njia ya kielektroniki ili tuweze kujua anayewajibika na asiyewajibika” Amesema Nzunda.


Nzunda amebainisha kuwa baada ya usajili huo, Maafisa ugani na wafugaji hao watawekwa kwenye mfumo ambao utairahisishia Serikali kufuatilia utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kufahamu mahali na  idadi ya wafugaji waliotembelewa na kuhudumiwa na Maafisa ugani hao na kupata mrejesho wa aina ya huduma waliyoipata kutoka kwa Maafisa ugani hao.


“Kwenye hili nitaanza mimi kisha ntawashawishi wenzangu wa Uvuvi, Kilimo na Maliasili ili twende pamoja kwa sababu ni lazima tufanye mabadiliko ya kuwabadili wafugaji, kuwaelimisha na kuchukua hatua za kuimarisha ufugaji nchini’ Ameongeza Nzunda.


Katika hatua nyingine Nzunda amesema kuwa Serikali imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha mashamba ya Mifugo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kupeleka mbegu bora za  ng’ombe wa nyama na maziwa.


“Mashamba yetu yalikuwa yanachechemea hivyo Serikali imeamua kuyaimarisha kwa kupeleka mifugo bora kwenye mashamba hayo ambapo  Shamba la Mabuki na Sao Hill tutapeleka Ng’ombe 500 kila moja na kule Kitulo tutapeleka ng’ombe wazuri wa maziwa 250, Ngerengere na Nangaramo ng’ombe 250” Amesisitiza Nzunda.


Mafunzo hayo kwa Maafisa Ugani yamefanyika katika kanda zote nchini lengo likiwa ni kuwakumbusha wataalam hao namna bora ya kutekeleza majukumu yao ili kuendana na Mpango kazi wa Miaka 5 wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi unaolenga kuboresha sekta ya Mifugo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mafunzo kwa Maafisa Ugani kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (hawapo pichani) tukio lililofanyika leo (17.11.2022) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Mafunzo kwa Maafisa Ugani kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (hawapo pichani) tukio lililofanyika leo (17.11.2022) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani (Mifugo) Bw. Samwel Mdachi akieleza lengo la Mafunzo kwa Maafisa Ugani kote nchini ikiwa ni muda mfupi kabla ya Ufunguzi wa Mafunzo ya Maafisa Ugani kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu kusini tukio lililofanyika leo (17.11.2022) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda (katikati, mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya Maafisa Ugani kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu kusini yaliyofanyika leo (17.11.2022) kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni