Nav bar

Jumatano, 19 Oktoba 2022

DKT. NAWANDA AWAPA KONGOLE MIFUGO NA UVUVI KWA VITUO ATAMIZI

◼️ Akoshwa na ufungashaji wa mazao ya Uvuvi 


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Yahaya Nawanda ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuanzisha vituo atamizi vinavyolenga kuongeza uboreshaji na uzalishaji wa mifugo nchini.


Mhe. Nawanda ambaye pia alikuwa mgeni rasmi kwenye Ufunguzi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji, Mkoani Simiyu ameyasema hayo muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Wizara hiyo ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wataalam waliohitimu taaluma za masuala ya Mifugo.


"Lakini nikikutana na Waziri wa Mifugo nw Uvuvi Mhe. Ndaki ntamshauri aangalie namna ya kupeleka baadhi ya vijana kule Busega kuna Taasisi kubwa sana ya vijana wenzao wanaofanya shughuli hii ya unenepeshaji na binafsi nipo tayari kuwagharamia malazi na chakula vijana 10 watakaochaguliwa kwenda kule" Amesisitiza Mhe. Dkt. Nawanda.


Mhe. Nawanda amesema kuwa hatua hiyo ya vijana kwenda kujifunza kwenye eneo ambalo shughuli za unenepeshaji zinaendelea itawasaidia kujifunza kwa vitendo jambo ambalo litawaongezea uelewa wa kile ambacho wanatakiwa kwenda kufanya baada ya kuhitimu mafunzo yao.


Akiwa kwenye eneo la Sekta ya Uvuvi Mhe. Dkt. Nawanda amefurahishwa na elimu ya usindikaji wa mazao ya uvuvi kabla hayajasafirishwa ambapo ametoa rai kwa wadau mbalimbali waliopo maeneo ya Kanda ya Ziwa kufika kwenye Maonesho hayo ili kupata elimu hiyo itakayowasaidia kufanya biashara ya mazao hayo kwa ufanisi.


"Nimefurahi sana kuona namna samaki alivyofungashwa kwa namna tofauti na jinsi dagaa walivyokaushwa kwa njia mbalimbali  hakika kazi inayofanywa na sekta ya Uvuvi ni kubwa" Ameongeza Nawanda. 


Aidha Mhe. Dkt. Nawanda ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla kuhakikisha wanakula kwa wingi vyakula vinavyotokana na mazao ya mifugo na Uvuvi katika nyakati tofauti ili kuongeza kiwango cha Protini katika miili yao na kupunguza changamoto ya udumavu.


Maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya Chakula Duniani hufanyika Oktoba 10-16 ya kila mwaka kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vyakula mbalimbali ili kuboresha afya ya mwili na akili na kwa mwaka huu yanaadhimishwa kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji, Mkoani Simiyu.

Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tumaini Chambua (kushoto) akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda (kulia) namna ya kusindika samaki kabla ya kuwasafirisha muda mfupi baada ya Mhe. Dkt. Nawanda kufika kwenye banda la Wizara hiyo lililopo kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji, Mkoani Bariadi yanakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani leo (11.10.2022)

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akionesha mmoja wa samaki aina ya Sangara aliowakuta kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanakofanyika Mkoani Simuyu. (11.10.2022)


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda (kushoto) akimueleza Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ugani (Mifugo) Bw. Samwel Mdachi namna Mkoa wake kupitia Wilaya ya Busega ilivyoanzisha kituo cha kunenepesha Mifugo muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji, Mkoani Bariadi yanakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani leo (11.10.2022).

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda akiangalia dagaa kutoka Ziwa Victoria waliokaushwa kwa jua muda mfupi baada ya kufika kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye Viwanja vya Halmashauri ya Mji, Mkoani Bariadi yanakofanyika Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani leo (11.10.2022).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni