Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imefanya tahmini ya utendaji kazi wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwa lengo la kupima utendaji kazi wake na kuona kama kuna changamoto zozote zinazokikabili kitengo hicho.
Akizungumza mara baada ya
kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo leo (07.09.2022) kilichofanyika katika
kumbi za bunge Jijini Dodoma, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki
amesema kuwa lengo la kukutana na kamati hiyo ni kutathmini majukumu na
utendaji kazi wa MPRU kama yanatekelezwa sawasawa.
Waziri Ndaki amesema kuwa
baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya MPRU na kujadiliwa,
kamati hiyo imetoa ushauri ambao Wizara itakwenda kuufanyia kazi ikiwa ni
pamoja na kukifanya kitengo cha MPRU kuwa taasisi kamili inayojitegemea ya
serikali. Lakini pia kamati imeshauri kuwa MPRU sasa ianze kusimamia maeneo
yote kwa maana ya bahari pamoja na maji baridi.
Hata hivyo Waziri Ndaki
ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuyatunza maeneo tengefu kwa kuwa maeneo
hayo hutumika kama mazalia ya samaki, hivyo watanzania kwa ujumla wanatakiwa
kuhakikisha wanayalinda maeneo hayo pamoja na kupiga vita uvuvi haramu kwa kuwa
ni moja ya chanzo cha uharibifu wa maeneo hayo.
Aidha, Waziri Ndaki amewataka
viongozi wa BMU kuhakikisha wanatimiza wajibu wao, kwani kumekuwa na tatizo kwa
baadhi ya viongozi hao kujihusisha na masuala ya uvuvi haramu. Hivyo Sekta ya Uvuvi
imejipanga kuhakikisha inawachukulia hatua viongozi wote ambao watabainika
kuhusika na uhujumu wa rasilimali za uvuvi.
Akizungumza wakati anafunga
kikao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe.
Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa kamati imepitia utendaji kazi wa MPRU na
imaona sasa umefika wakati wa kitengo hicho kuwa taasisi kamili hivyo Wizara
iendelee na mchakato wa kulikamilisha hilo.
Katibu Mkuu anayesimamia
Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa MPRU imekuwa ikifanya kazi
toka mwaka 1994. Majukumu yake makubwa ni kutambua maeneo ya kuhifadhi,
kuyasimamia na kuyaendeleza. Kamati imeweza kufahamishwa muundo na majukumu ya
MPRU na kwamba sasa inatakiwa kuwa taasisi kamili hivyo kuna mabadiliko ambayo yatahitajika
kufanyika hadi kwenye sheria iliyoanzisha kitengo hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) akifunga kikao cha kamati hiyo kilichopokea taarifa ya muundo na majukumu ya Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) ambapo amesema kuwa taarifa hiyo ifanyiwe marekebisho kulingana na ushauri uliotolewa na kamati ili taratibu nyingine ziweze kuendelea. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. (07.09.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati Sekta ya Uvuvi ilipowasilisha taarifa ya muundo na majukumu ya Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwa kamati hiyo. Mhe. Ndaki amesema kuwa lengo ni kuhakikisha uhifadhi unafanyika kwenye bahari pamoja na maziwa, lakini pia ameisihi jamii kushirikiana na serikali katika kuhifadhi maeneo tengefu kwa kuwa ni mazalia ya samaki. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb). (07.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya muundo na majukumu ya Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwa kamati hiyo. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. (07.09.2022)
Meneja wa Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Bw. John Komakoma akiwasilisha taarifa ya muundo na majukumu ya Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kikao hicho kimefanyika bungeni Jijini Dodoma. (07.09.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni