Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi Umoja wa Vijana Taifa Cde. Victoria Mwanziva amefanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki kuhusu nafasi ya vijana katika sekta hizo za uzalishaji.
Mazungumzo hayo yalifanyika jana
(07.09.2022) kwenye ofisi za Wizara zilizopo kwenye jengo la NBC Benki Jijini
Dodoma wakati Mwanziva alipomtembelea Waziri Ndaki.
Lengo kuu la Katibu wa
Uhamasishaji limekua ni kupata mrejesho wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alilotoa wakati akifunga Maonesho
ya NaneNane 2022 mkoani Mbeya juu ya namna gani vijana wanaweza kunufaika na
sekta ya ufugaji na uvuvi.
Waziri Ndaki amemhakikishia Katibu
huyo kuwa tayari serikali imekwishafanya maandalizi ya mpango maalumu ambapo
vijana 240 watapelekwa kwenye vituo atamizi na kuwa chini ya usimamizi wa
wataalam wakitumia teknolojia mpya ya ufugaji na sayansi ya unenepeshaji na
mara baada ya kuhitimu kila mmoja atapatiwa ng’ombe 10 kama mtaji wa
kujiendeleza. Bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hili tayari ipo hivyo
taratibu zinaendelea, na idadi ya vijana itaendelea kuongezeka kulinga na
bajeti itakavyoruhusu.
Katika hatua nyingine, Waziri
Ndaki amemweleza kuwa upande wa uvuvi serikali inaandaa vizimba zaidi ya 800
upande wa Ziwa Victoria ambapo hii inamlenga kijana kujihusisha na ufugaji wa
samaki kibiashara na serikali inagharamia hatua zote zilizokua zikimkwamisha
kijana ikiwa ni pamoja malipo ya tathimini ya mazingira na gharama za NEMC
ikiwa ni pamoja na eneo.
Kwa ukanda wa pwani Serikali
inakwenda kuleta Boti za kisasa (Fiber Boats) ambapo jumla ya Boti 240
zitakopeshwa kwa vijana na makundi mbalimbali. Uwezeshwaji na ukopeshaji;
uratibu na usimamizi utafanyika chini ya Halmashauri husika ambazo zitakuwa na
utekelezaji wa programu hizi.
Mwisho Waziri Ndaki amesisitiza kuwa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), serikali imewekeza fedha za kutosha kwa vijana kukopeshwa bila riba na kuwaomba wajitokeze na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hii kupitia halmashauri zao akihimiza Maafisa Uvuvi kufikisha taarifa hizi kwa Vijana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni