Nav bar

Jumapili, 14 Agosti 2022

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAANZA UTEKELEZAJI WA MAAGIZO YA MHE. RAIS SAMIA

Na Mbaraka Kambona,


Kufuatia maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za Wakulima (NaneNane) Agosti 8, 2022 jijini Mbeya ya kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kuwezesha vijana kujiajiri katika sekta ya mifugo na kufanya maboresho makubwa ya utendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Wizara imeanza kuchukua hatua mbalimbali za utekelezaji wa maagizo hayo.


Akitoa taarifa kwa umma mapema leo jijini Dodoma Agosti 12, 2022, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema kuwa wameshaanza kutekeleza maagizo hayo na mwaka huu wa fedha 2022/23 Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) imeanzisha vituo atamizi nane (8)  ambavyo vitahusisha vijana 240 waliohitimu taaluma za mifugo kwa ajili ya unenepeshaji mifugo katika vituo hivyo vilivyopo katika mikoa ya Tanga, Kagera, Songwe na Mwanza.


"Nimeziagiza taasisi hizo kuanza ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya unenepeshaji wa mifugo mara moja na kukamilisha taratibu za kuwapatia vijana", alisema Ndaki


Alisema kuwa ili kufanikisha hilo Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wahitimu wajasirimali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanaofahamika kama SUGECO, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya CRDB, Viwanda vya kuchakata mazao y mifugo nchini, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Dhamana ya Uwezeshaji Kilimo (PASS) na NARCO.


Aliongeza kuwa baada ya kupitia mikataba na mipango ya kibiashara kwa kila mwekezaji katika vitalu vya NARCO watatenga vitalu vya unenepeshaji wa mifugo kwa ajili ya kuwapangisha vijana hao watakaohitimu katika vituo hivyo  atamizi.


Kuhusu tathmini ya upangishaji wa vitalu vya NARCO, Mhe. Ndaki alisema kuwa Wizara imeunda timu ya Wataalam kutoka Serikalini na taasisi mbalimbali za sekta binafsi kufanya tathmini ya kina ya Utendaji na changamoto zinazoikabili Kampuni hiyo ili waweze kuishauri vizuri Serikali. 


Aidha, aliongeza kwa kusema kuwa NARCO inafanya mapitio ya mikataba na mipango ya biashara kwa kila mwekezaji kulingana na mikataba yao ili kubaini hali halisi ya uwekezaji.


Ili uwekezaji wenye tija katika Ranchi za NARCO uweze kufanyika kikamilifu, Waziri Ndaki alisema NARCO imeainisha na kutenga vitalu vitano (5) vyenye ukubwa wa takriban hekta 32,500 ili kuvutia wawekezaji mahiri na wenye mitaji kutoka ndani na nje ya nchi.


Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki alitoa wito kwa wafugaji na wavuvi wote nchini kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti 23, 2022.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni