Nav bar

Jumapili, 14 Agosti 2022

RAIS SAMIA ATAKA WANANCHI WAFUNDISHWE UFUGAJI KIBIASHARA.

Na. Tajiri Kihemba, IRINGA.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Wananchi wapewe Elimu juu ya Ufugaji kibiashara kwa kuzingatia mahitaji ya soko ili kupata manufaa makubwa.


Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza hayo leo Agosti 12,2022 alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Iringa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Samora Mkoani Iringa.


"Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa Mikoa inayoshughulika na ufugaji pia, ripoti ya Mkoa inaonesha Mkoa una jumla ya Ng'ombe 348,846 Mbuzi 183,180 na Kondoo 69,894 na katika eneo hilo Wafugaji ni muhimu sana, Wananchi waelekezwe kufuata kanuni za ufugaji bora na waendelee kuelimishwa ufugaji kibiashara kwa kuzingatia mahitaji ya soko ili kupata manufaa makubwa." Amesema Rais Samia Suluhu Hassan


Rais Samia Suluhu Hassan pia ameziagiza Halmashauri Nchini kutenga maeneo kwa ajili ya Wakulima na Wafugaji ili kuondoa migogoro inayoweza kutokea baina ya Wakulima na Wafugaji.


"Changamoto katika Sekta ya Mifugo Nchini ni pamoja na migogoro kwenye matumizi ya Ardhi, kwa kuwa Mkoa wa Iringa bado hauna migogoro ya aina hii na ili migogoro hii isijitokeze nazielekeza Halmashauri zitambue maeneo yote ya malisho na kuyapima ili kupunguza muingiliano wa matumizi ya Ardhi, na kwa kufanya hivyo tutapunguza migogoro ya Ardhi kati ya Wafugaji na Wakulima." Amesema Rais Samia Suluhu Hassan.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan atahitimisha ziara yake Mkoani Iringa kesho Tarehe 13/08/2022 kwenye Jimbo la Isimani kwa Mhe. William Lukuvi (MB).



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni