Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema nchi ya Oman imedhamiria kuwekeza kwenye biashara ya mifugo nchini Tanzania.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo (15.08.2022) baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman Nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidhani wakati alipofika kwenye ofisi za Wizara zilizopo kwenye mji wa Serikali – Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri Ndaki amesema haya yanatokea kutokana na Safari ya
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan nchini Oman pamoja na mazungumzo yaliyofanyika
kati ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na Mamlaka ya Uwekezaji ya nchi ya
Oman, hivyo mazungumzo yaliyofanyika ni kuona hatua gani ya utekelezaji
iliyofikiwa ili kuhakikisha mazungumzo yaliyofanyika yanatekelezwa.
Wizara kupitia Sekta ya Mifugo imemueleza Mhe. Balozi
maeneo mbalimbali ya uwekezaji kupitia Sekta hiyo ikiwemo uwekezaji kwenye
Machinjio, Viwanda vya Nyama na Ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi,
Uzalishaji wa Malisho na Chakula cha Mifugo.
Lakini nchi ya Oman imeonesha nia kwa kuanza kufanya
biashara ya mifugo hai kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) hivyo kupitia
mazungumzo yaliyofanyika Wizara inategemea ifikapo Oktoba mwazoni biashara hiyo
inaanza kufanyika.
Waziri Ndaki amesema kuwa hii ni fursa kwa watanzania kwa
kuwa mifugo hai itakayokuwa inauzwa sio ya Kampuni ya NARCO peke yake bali watanunua
mifugo kutoka kwa wafugaji wengine, hivyo wafugaji wahakikishe wanatunza mifugo
yao kulingana na maelekezo wanayopewa na wataalam ili kuzalisha mifugo iliyo
bora.
Kupitia uwekezaji wa Nchi ya Oman kwenye biashara ya
mifugo, wafugaji watapata soko la uhakika, uhakika wa bei nzuri mifugo pamoja
na mazao ya yake, hivyo wafugaji wajipange kufuga kibiashara na kuhakikisha wanavuna
mifugo kulingana na maeneo ya malisho waliyonayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe amesema kuwa biashara itakayofanyika ni ya ng’ombe kati ya 3,000 hadi 4,000 kwa mwezi. Aidha, amesema kuwa Kampuni ipo tayari kufanya biashara kwa kushirikiana na wafugaji kuhakikisha biashara ya mifugo kati ya Tanzania na Omani inafanyika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akizungumza kwenye kikao kifupi na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidhani (kushoto) ambaye alifika kwenye ofisini za Wizara zilizopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba kuzungumzia nia ya nchi yao kuwekeza kwenye biashara ya Mifugo hapa nchini kupitia Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Waziri Ndaki amemuhakikishia Mhe. Balozi kuwa Wizara kupitia (NARCO) itatoaa ushirikiano unaohitajika kuhakikisha biashara ya mifugo baina ya nchi hizo mbili inafanikiwa na kuleta maendeleo kwa wafugaji na taifa kwa ujumla. Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. (15.08.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifafanua jambo wakati wa kikao kifupi cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidhani (hawapo pichani) kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara uliopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba. (15.08.2022)
Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda (wa pili kulia waliokaa mstari wa mbele) pamoja na viongozi kutoka Sekta ya Mifugo na Ubalozi wa Oman Nchini Tanzania wakifuatilia wasilisho kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya mifugo nchini Tanzania kwenye kikao kifupi kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara uliopo kwenye Mji wa Serikali – Mtumba. (15.08.2022)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Mifugo, Mhe. Abdallah Ulega (wa tatu kutoka kulia), Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Mhe. Tixon Nzunda (wa kwanza kushoto mbele), Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud Al Shidhani (wa pili kushoto) na baadhi ya Viongozi wa Wizara Sekta ya Mifugo pamoja na Viongozi kutoka Ubalozi wa Oman Nchini Tanzania mara baada ya kumaliza kikao kifupi kilichojadili uwekezaji wa nchi hiyo kwenye biashara ya mifugo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara , Mji wa Serikali - Mtumba. (15.08.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni